Tuesday, 14 June 2016

WABUNGE 6 NCHINI KENYA WATIWA MBARONI KWA KUTOA KAULI ZA CHUKI














Miongoni mwa wabunge hao, wamo watatu wa chama tawala cha muungano wa Jubilee na wanne wa vyama cha upinzani kupitia muungano wa Cord akiwemo seneta mmoja.
Wabunge wa chama tawala ni pamoja na Moses Kuria, Kimani Ngunjiri na Ferdinand Waititu huku wale wa upinzani wakiwa ni pamoja na Junet Mohammed, Aisha Jumwa, Johnson Muthama na Seneta Timothy Bosire.

Inadaiwa kuwa siku ya Jumapili iliyopita mbunge wa Jubilee Moses Kuria alirekodiwa sauti yake iliyokuwa katika lugha ya Kikuyu akisema “Kama kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga angekuwa ameuawa, matatizo yote ya wakenya yangekuwa yamemalizika”

Wabunge wengine wa Jubilee pia wanatuhumiwa kwa kutoa kauli za kuunga mkono kauli hiyo.
Kwa upande wa wabunge wa Cord, wao wanatuhumiwa kwa kuitisha mkutano na vyombo vya habari na kuwataka wafuasi wa vyama hivyo vya upinzani kufanya jukumu la kumlinda kiongozi wao Raila Odinga, kwa madai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa kufanya kazi hiyo.

Jeshi la polisi nchini humo limetafsiri kauli hizo kuwa ni kauli za kueneza chuki, na hivyo limewahoji na litawachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Hali ya kisiasa nchini Kenya haijatulia kufuatia vuguvugu la vyama vya upinzani chini ya kiongozi wao Raila Odinga kutaka mabadiliko yafanyike katika Tume ya Uchaguzi nchini humo, matakwa ambayo serikali imesema haitayatekeleza na hivyo kusababisha maandamano ya mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment