Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Sospeter Muhongo amelishauri Baraza la Wafanyakazi wa Nishati na Madini kujikita katika kujadili mwelekeo wa mapinduzi ya kiuchumi kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwanda.
Mhe. Muhongo aliyasema
hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Baraza la
Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambapo baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika kikao
hicho ni masuala ya usafiri kwa wafanyakazi wa wizara hiyo, upandishwaji vyeo
kwa wafanyakazi, mafunzo pamoja na uhaba wa nafasi wa ofisi kwa wafanyakazi.
Kuhusu suala la
upandishwaji vyeo, Mhe. Muhongo alisema kuwa tayari yeye kama Waziri
alishafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ili kuona namna gani
wafanyakazi wanapandishwa vyeo kulingana na elimu pamoja uwezo wao kikazi
ambapo alipendekeza kubadili mtindo wa upandishwaji vyeo uliopo sasa kwani ni
wa zamani.
‘’Sifa za upandishaji vyeo kwa wafanyakzi ni vema ukabadilika pamoja na
muda wa utoaji vyeo, hivyo napenda kuwasisitiza kuwaangalia vijana tulio nao
kwani pale Wizarani tuna vijana wengi wazuri wenye uwezo mkubwa katika kufanya
kazi. Katika kikao hiki ni vema mkajadili namna gani mnawapa kipaumbele vijana
katika kuwapandisha vyeo vijana hawa,’’ alisema Muhongo.
Kuhusiana na uhaba wa
nafasi za ofisi, Mhe. Muhongo alifafanua kuwa, ofisi nyingi za Serikali ziko
katika mfumo wa zamani, hivyo amelishauri Baraza hilo kuona namna gani
watabadilisha muundo wa ofisi ili watu wakae pamoja katika eneo moja lililo
wazi na kufanya kazi kuliko kila mtu kuwa na sehemu yake ya kufanyia kazi hali
inayosababisha ufinyu wa eneo na uvivu.
Aidha, Amewataka
wajumbe wa Baraza hilo kujadili ni namna gani wanaweza kubadilisha hali ya
kiuchumi toka asilimia 7% hadi kufikia asilimia 8% mpaka 10% ili kukuza uchumi
wa nchi na kutokomeza umasikini.
‘’Jukumu kubwa la Wizara ya Nishati na Madini
ni kuhakikisha kuwa tunakuza uchumi wa nchi kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na
umeme mwingi wa bei nafuu na wa uhakika, na kazi tuliyonayo hapa ni kuongeza
uzalishaji wa umeme toka Megawati 1400 hadi kufikia Megawati 5,000 mpaka 10,000
na ikiwezekana hadi 15,000 baada ya miaka 10 ijayo’’, aliongeza Mhe. Mhongo.
Kuhusu suala la
Mafunzo kwa wafanyakazi hao, Mhe. Muhongo alisisitiza kuwa hakuna mtu
anayekatazwa kupatiwa mafunzo kwa maana ya kuongeza elimu juu ya jambo fulani,
isipokuwa kuna utaratibu wa kwenda kusoma, ambapo panapotokea umuhimu wa
wafanyakazi kwenda kusomea mambo muhimu yenye manufaa kwa umma nafasi hizo ni
vema zikatolewa ili nchi iwe na wataalam mbalimbali katika nyanja mbalimbali.
‘’Hii Wizara inahitaji watu wasome na
waelimike, hivyo tunahitaji watu wasome na wawe wataalam katika maeneo
mbalimbali ya kazi lengo likiwa ni kuleta maendeleo ya nchi’’, Alisema Mhe. Muhongo.
Aligusia masuala ya
Bajeti katika Wizara yake ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 89.5/% ya
bajeti itatumika katika kufanya shughuli za maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment