Tuesday, 19 April 2016

RAISI JOHN POMBE MAGUFULI AMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM WILSON KABWE



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Wilson Kabwe kuanzia leo tarehe 19.04.2016.

 Rais amefikia uamuzi huo leo wakati akitoa hotuba ya uzinduzi wa Daraja la Kigamboni ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amemueleza Rais Magufuli kwamba Mkurugenzi huyo alisaini mikataba ya kuliingizia taifa hasara katika stendi ya ubungo na 'Packing' jijini Dar es salaam.

''Mkataba wa mwaka 2004 ulitaka kila basi litozwe shilingi elfu 4 kila linapotoka kituoni ambapo mwaka 2009 Kabwe alisaini mkataba ambao ulitaka kila basi litozwe shilingi elfu 8 jambo ambalo halikutekelezwa kwa kipindi chote hadi sasa na kusababisha hasara ya bilioni 3'' Alisema Makonda.

Makonda pia ameongeza kuwa Mkurugenzi huyo vilevile amekiuka sheria ya kutoa dhabuni baada ya anayefanya kazi ya kutoza kodi za 'packing' katika jiji la Dar es salaam kumaliza muda wake lakini Mkurugenzi alimuongezea muda wa miezi minnekwa barua na baadaye miezi 6 kwa kisingizio kwamba mchakato unaendelea wa kumpata mtu mwingingine bila ya kutangaza dhabuni jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Kufuatia maelezo hayo Rais Magufuli amesema viongozi wazembe hawatakuwa na nafasi katika serikali yake ili kuhakikisha maendeleo ya kweli kwa watanzania yanapatikana.
''Sitakuwa na simile pakitokea jipu sitasubiri nitalitumbua nikisubiri litazidi kuwa na usaha'' -Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza jambo hilo ili kubaini ukweli wa mambo ili sheria ichukue nafasi yake.

No comments:

Post a Comment