Kamanda wa
Polisi, Justus Kamugisha.
Serikali
imepangua uongozi wa vyombo vya dola mkoani Mwanza kwa kuwahamisha vituo vya
kazi watendaji wakuu akiwamo Kamanda wa Polisi, Justus Kamugisha aliyehamishiwa
mkoani Mbeya.
Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza John Mongella alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa taasisi
hizo na kukabiliana na matukio ya uhalifu yaliyotikisa mkoa huo tangu kuanza
kwa mwaka huu.
“Kwa
kipindi kifupi cha wiki mbili tangu nihamie Mwanza, nimeshuhudia matukio kadhaa
ya uhalifu, yakiwamo mawili ya ujambazi yaliyoishia kwa raia wema kupoteza
maisha na mamilioni ya fedha kuporwa,” alisema Mongella. “RPC amehamishiwa
Mbeya ambako nadhani labda kuna changamoto kidogo kulinganisha na zile za
Mwanza alizoonyesha kushindwa,” alisema Mongella.
Mongella
alisema pamoja na RPC, vigogo wengine waliohamishwa kutoka Mwanza ni pamoja na
ofisa utumishi wa jeshi la polisi, ofisa Idara ya Usalama wa Taifa na kamanda
wa mkoa wa Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza
na viongozi, watumishi na watendaji wa vyombo vya dola wilayani Magu, Mongella
aliwataka kutimiza wajibu kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya uhalifu
katika maeneo yao, akionya watakaoshindwa watawajibishwa.
“Haiwezekani
majambazi yatambe kwa kuvamia, kupora na kuua wananchi watakavyo, na vyombo vya
dola na viongozi wenye dhamana ya ulinzi na usalama wapo wanashuhudia. Kila mtu
atimize wajibu wake,” alisema Mongella.
Alitumia
fursa hiyo kuuagiza uongozi wa polisi wilaya ya Magu kukomesha matukio ya
mauaji ya kukata watu kwa mapanga yanayodaiwa kufanywa na watu wanaodishwa.
Ndani ya
kipindi cha miezi miwili ya Februari na Machi, Jiji la Mwanza limekumbwa na
matukio sita ya ujambazi ambayo yamechukua maisha ya watu sita waliouawa kwa
kupigwa risasi, huku mamilioni ya fedha yakiporwa kutoka maduka ya fedha kwa
njia ya mitandao.
Msemaji wa
polisi, Advera Bulimba ambaye awali hakupatikana kuzungumzia suala hilo alituma
ujumbe wa simu akieleza kuwa RPC wa Mwanza ni Ahmed Msangi, kwa upande wake
Kamanda Kamugisha hakupatikana ila Msangi, ambaye alikuwa kamanda wa Mbeya naye
alithibitisha uhamisho huo.
“Ni kweli
nimehamishiwa Mwanza na nitafika wakati wowote,” alisema Kamanda Msangi
alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi jana.
Akizungumzia
matukio hayo, Mchungaji wa Kanisa la Gosheni Inland Church, Hosea Mjulizi,
ambaye ni mkazi wa Igogo, alisema baadhi yanayotokea ni kutokana na vyombo vya
dola na viongozi kupuuza taarifa zinazotolewa na wananchi.
“Mfano hai
ni Kata ya Igogo ambayo ni kati ya maeneo yanayoongoza kwa uhalifu jijini
Mwanza. Licha ya wahalifu kujulikana kwa majina, nyumba zao na matukio
waliyohusika, hawachukuliwi hatua,” alisema Mchungaji Mjulizi.
Alisema
kwa nafasi yake ya uongozi wa kiroho, alifanya mikutano kadhaa na vijana
wanaotuhumiwa kujihusisha ambao walikuwa tayari kujisalimisha, lakini viongozi
wa eneo hilo na Jeshi la Polisi hawakutoa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment