Thursday 28 April 2016

MAJAMBAZI YAUA WAWILI MKOANI GEITA

Watu 2 wameuawa kwa kupigwa  na majambazi waliokuwa  wamevamia katika  baa  inayofahamika kwa  jina la High way pub iliyoko mtaa wa Mwatulole kata ya Buhalahala mkoani Geita.

Akithibitisha kutokea  kwa tukio   hilo mratibu mwandamizi  wa polisi Isack Msengi  amesema kuwa tukio hilo  limegunduliwa na msimamizi  wa  ulinzi  wa kampuni  ya Mara Security Didas John alipokuwa akikagua lindo baada ya kufika kazini mapema hii leo ndipo  alipogundua kuuawa kwa  watu hao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mratibu mwandamizi huyo inadaiwa kuwa  majambazi hao walianza kumuua  mlinzi wa baa hiyo bw, Yusuph Kilanga 38 mkazi wa Kivukoni kwa kumpiga na kitu kizito kichwani  na baadae kuvunja dirisha la kaunta na  kumuua msimamizi wa baa hiyo  Jermiah Elias 19 mkazi wa Mwatulole kisha kumuingiza ndani alipokuwa amelala .

Baada ya kufanya mauaji hayo majambazi hao walichukua pesa kiasi cha sh. laki 4  zilizokuwa kaunta na baadae  kuvunja duka la sementi lililopo jirani na eneo hilo na kuiba kiasi cha shilingi milioni 1, kisha kutokomea nazo kusikojulikana.

Katika eneo la tukio kumepatikana Msumeno mmoja mdogo na Fyekeo moja ambapo hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi  ili kuwabaini wahusika wa mauaji hayo.


No comments:

Post a Comment