Sunday, 26 November 2017

RAIS MAGUFULI ATEMBELEA BANDARI LEO NA KUTOA MAAGIZO


Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa Mamlaka ya Mapato( TRA), Mamlaka ya Bandari(TPA), TAKUKURU na Wizara ya Fedha kuhakikisha inatoa taarifa ni nani alihusika kuagiza magari 50 kupitia mgongo wa Ofisi ya Rais.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Jumapili Novemba 26 baada ya kufanya ziara ya ghafla bandarini mara baada ya kutembelea meli ya Wachina iliyofanya matibabu kwa Watanzania kwa muda wa siku 5.

Magari hayo aina ya ambulance ambayo mpaka leo yapo bandarini, yaliagizwa mwaka 2015 kupitia majina ambayo hayatambuliki na Ofisi ya Rais.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais amewahoji IGP, Waziri wa Fedha, Kamishna Mkuu wa TRA na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ambao hata hivyo hawakuwa na mujibu kuhusu nani hasa mwagizaji wa magari hayo.

“Natoa onyo kwa mawaziri na wateule wale wote waliotangaza, sitaki mpaka nije kubaini uozo mimi mwenyewe ninataka mpigane kuhakikisha uozo wote unaondoka, safari nyingine nikigundua jambo lolote na wewe ni eneo lako hautapona,” amesema.

Ameongeza, “Ninatoa siku saba, nataka aliyeagiza haya magari kwa mgongo wa Ofisi ya Rais atambulike ni nani na ninatoa maagizo hata kama ni mtu mkubwa kiasi gani atambulike nahitaji mujibu.”

Wakati huohuo Rais Magufuli ametembea umbali wa zaidi ya mita 700 ili kukagua magari ya polisi ambayo yaliingizwa nchini mwaka 2015 lakini bado zaidi ya magari 50 yameendelea kubaki eneo la bandari.

No comments:

Post a Comment