Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ameungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo pamoja na mambo mengine amewahusia watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.
"Niwaombe watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote tumtangilize Mungu mbele.
"Wakati
tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu
Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo
ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane" Amebainisha Rais
Magufuli
Pamoja na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ibada
hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga
na Mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni familia rafiki wa Rais Magufuli, waliowasili
hapa Chato jana jioni Tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko wakitokea Nairobi,
Kenya.
Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Mheshimiwa
Odinga amewashukuru watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na wakenya, huku
akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Mheshimiwa Odinga ametoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu
Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu
kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya
kukataa kumpa pasi hiyo.
Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema
urafiki huo ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na
yeye kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa
walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa
barabara, na kwa umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na waasisi Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere wa Tanzania, Jalamogi Odinga wa Kenya na Milton Obote wa
Uganda.
No comments:
Post a Comment