Wanawake wapato elfu 70 wanaoishi
katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa dhahabu mkoani Geita wanalengwa
kujengewa uwezo wa kiuchumi pamoja na kupatiwa huduma bora za afya.
Hayo yamesemwa na mratibu wa mradi wa The
Golden Line,Bi Violet Alphonce unaotekelezwa na chama cha uzazi na malezi bora
Tanzania UMAT ambalo ni shirika lisilo la kiserikali kwa kushirikiana na Health
Enterpreneur na Solidaridad.
Ufafanuzi huo umetolewa wakati wa kikao cha
majadiliano ya utekelezaji mradi huo baina ya shirika hilo na madiwani wa kata
tano zinazopatikana katika halmashauri ya mji Geita,halmashauri ya wilaya ya
Bukombe na halmashauri ya wilaya Geita.
Mratibu huyo amesema mradi wa The Golden Line
unampelekea mwanamke huduma za uzazi salama,uzazi wa mpango,huduma ya magonjwa
ya saratani ya shingo ya kizazi na zaidi kumpunguzia mwanamke kutembea umbali
mrefu kufuata huduma hizo za uzazi.
Bi Violet aidha katika suala la kumuinua
mwanamke kiuchumi amedai kuwa shirika hilo linapigania usawa na kuona mwanaume
na mwanamke wote kwa pamoja wananufaika na rasilimali ya dhahabu katika maeneo
ya uchimbaji.
Nao baadhi ya madiwani kutoka kata 5 za
Katente,Nyaruyeye,Lwamgasa, Nyarugusu na Mgusu ambapo mradi huo
unatekelezwa wamedai kuridhishwa na mradi huo na kuahidi kushirikiana kuwapa
huduma wananchi wao.
The Golden Line kwa maana ya mstari wa dhahabu
ni mradi unaotekelewa kwa miaka 5 na mpaka sasa wanawake zaidi ya elfu 5 wamekwishafikiwa
na mradi huo.
No comments:
Post a Comment