Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli,
itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa nguvu zote bila
kutetereka.
Lengo la hatua hiyo ni kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya
Serikali na kuboresha uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa rasilimali za
umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema hayo katika hotuba
yake kwa Taifa wakati wa sherehe ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hivyo aliwaomba Watanzania wote kuunga mkono kwa vitendo juhudi
na maelekezo ya Dk Magufuli za hatua anazozichukua dhidi ya vitendo vya rushwa
na ufisadi nchini.
Kutokana na hatua hizo, Makamu wa Rais alisema hadi sasa jumla
ya kesi 596 za rushwa zinaendelea mahakamani na jumla ya Sh 6,543,342,793
tayari zimeokolewa.
“Naomba nitumie fursa
hii kuwakumbusha Watanzania wenzangu kujiepusha na vitendo vya kutoa na kupokea
rushwa,” alisema Samia na aliwataka watumishi wa umma,
watumishi katika sekta binafsi, wajasiriamali na kila mmoja kujiepusha na
vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria,
kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa.
“Kama
nilivyokwishasema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinaendelea kuhimiza
mapambano dhidi ya Rushwa chini ya kaulimbiu “Timiza Wajibu wako, kata Mnyororo
wa Rushwa,” aliongeza Makamu
wa Rais.
Samia alisema suala la rushwa limeongelewa mara nyingi na athari
zake zinajulikana ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa mali za umma, mikataba
isiyofaa kwa taifa na udanganyifu na kupokea fedha ili kukiuka sheria kwa
manufaa binafsi huchangia kwa kiwango kikibwa kuwanyima wananchi hazi zao na
kudhoofisha ustawi wa taifa letu.
Mbali na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendelea na
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pia alisisitiza kwa mara nyingine kwa
kusema kuwa Serikali haina nia ya kumwonea mtu inapochukua hatua ya kutumbua
majipu kwa watumishi wa umma.
Akishangiliwa na wananchi wakati akiwahutubia kwenye sherehe
hizo, Makamu wa Rais alisema lengo la Serikali la kutumbua majipu ni
kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini kama
ilivyoagizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote
wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mnasikia katika
Serikali ya Awamu ya Tano tunarekebishana, majipu yanatumbuliwa ...kwa kweli
hatuna nia ya kumwonea mtu, tunarekebishana na hilo ndilo lililomo katika agizo
ya Ilani yetu ya CCM ili kuwanufaisha Watanzania wote wafaidi matunda katika
nchi yao,”alisema Makamu wa
Rais.
No comments:
Post a Comment