Suala la mshahara wa Rais, limeibuka tena bungeni ambapo Bunge
limeelezwa kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais
hawezi kujipunguzia mshahara pindi anapoapishwa kushika wadhifa huo.
Hayo yalisemwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene,
kupitia taarifa aliyoitoa kwa Bunge baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo
Peneza (Chadema) kumuomba Rais John Magufuli kujipunguzia mshahara.
Mbunge huyo aliyasema hayo wakati akijadili Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa 2016/17 hadi 2021, ambapo pamoja na kusifu jitihada za Rais
Magufuli kwa kuonesha dhamira ya wazi ya kuwajali wananchi masikini na
kudhibiti matumizi ya serikali, alimuomba kupunguza mshahara wake na pia
kuruhusu ukatwe kodi.
“Kwa kweli kwa dhati
kabisa nampongeza sana Rais Magufuli kwa namna anavyoonesha wazi kwamba ana
dhamira ya kuwatumikia Watanzania. Kwa namna anavyokwenda ni wazi kwamba Rais
Magufuli anakuwa Rais wa pili kuwa na mapenzi ya dhati kwa Watanzania baada ya
Rais Nyerere (Julius- Baba wa Taifa).
“Pamoja na hayo, kama
anataka awe kama Mwalimu Nyerere basi ni wakati sasa wa Rais Magufuli kuchukua
hatua za kujipunguzia mshahara wake na pia kuruhusu mshahara wake kukatwa kodi,
hili litampa heshima kubwa sana Rais wetu,” alisema Peneza.
Akitoa taarifa kwa Bunge, Waziri Simbachawene alisema kwa mujibu
wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na
marekebisho yake, Ibara ya 43, Ibara ndogo ya 3, Ukurasa wa 62 inamzuia Rais
kupunguza mshahara akiwa madarakani.
Alisema; “Ibara
hiyo inasema hivi: ‘Mshahara na malipo ya Rais, havitapunguzwa wakati Rais
anapokuwa bado anashika madaraka yake.
“Rais aliyepo sasa hawezi
kujipunguzia mshahara wake yeye mwenyewe isipokuwa anapoondoka anaweza kuweka
kiwango cha mshahara cha Rais ajaye.
"Kwa hiyo wakati
wabunge mnaendelea kumuomba Rais apunguze mshahara wake ni lazima mjue jambo
hilo ni kinyume cha Katiba”.
Ufafanuzi huo wa Waziri umekuja siku chache wakati Rais Magufuli
akiwa tayari amejitangazia mbele ya umma kiwango cha mshahara anacholipwa
akisema ni Sh milioni 9.5 kwa mwezi.
Rais aliyasema hayo akiwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita
wakati alipokwenda kwa mapumziko mafupi hivi karibuni, hatua ambayo ilipokelewa
kwa shangwe na wananchi wengi
No comments:
Post a Comment