Tanzania imetajwa kuwa
inaongoza kwa kulima na kuzalisha ufuta Afrika huku ikishika nafasi ya tatu ya
duniani.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na
Maendeleo, Naliendele, Dk Omary Mponda, alisema kuwa Tanzania imefikia hapo
baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na serikali.
Jitihada hizo
zinafanyika kupitia watafiti wake wa masuala ya kilimo kwa kutafiti na kugundua
mbegu bora zinazostahimili ukame, magonjwa na wadudu.
Mtaalamu huyo ambaye
pia ni mtafiti kiongozi na mratibu wa mbegu za mafuta, alisema kwa sasa
Tanzania inazalisha wastani wa tani 460,000 kutoka tani 38,000 zilizokuwa
zikizalishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Alisema kwa mujibu wa
Shirika la Chakula Duniani (FAO), Tanzania imepanda kutoka nafasi ya saba
kidunia mwaka 1998 hadi kufikia nafasi ya tatu ikitanguliwa na India na Mayama.
“Hiki kituo cha utafiti kilianza mwaka 1945
wakati huo kilikuwa kinashughulikia korosho peke yake, lakini kufikia mwaka
1978 tulianza kuingiza utafiti wa mbegu za karanga na ufuta ambapo mpaka sasa
tumeshagundua mbegu aina 12 ambazo wakulima wetu wanazitumia”,alisema.
Mtaalamu huyo
aliyebobea katika masuala ya utafiti wa mbegu za mafuta, alisema kuwa zao hilo
miaka ya nyuma lilikuwa linalimwa katika mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara,
Lindi na Ruvuma. Alisema kutokana na hamasa kubwa inayofanywa na wataalamu wa
kilimo, tayari mikoa kadhaa inalima zao hilo.
“Huko nyuma hata eneo lililokuwa likilimwa
ufuta lilikuwa dogo sana, lakini sasa ni zaidi ya hekta 650,000 zinalimwa ufuta
nchi nzima…sasa haya ni mafanikio makubwa na yanayopaswa kujivunia na hiyo
inatokana na ugunduzi huu wa mbegu bora”, alisema.
Ufuta ni moja kati ya
mazao yanayoongeza kipato kwa makusanyo ya ndani kwa baadhi ya halmashauri za
wilaya ikiwemo wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi ambapo kwa
mujibu wa takwimu zilizopo Ruangwa, msimu uliopita ilipata Sh milioni 400
kutokana na ushuru wa mauzo.
No comments:
Post a Comment