Monday, 12 December 2016

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU MGENI RASMI UZINDUZI WA MPANGO WA KUZUIA UNYAYASAJI KIJINSIA



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika  uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2017-22) wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Hayo yamesemwa jana  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto (Maendeleo ya Jamii) Bi. Siaba Nkinga katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo alisema uzinduzi huo unatarajia kufanyika Desemba 13 mwaka huu Jijini Dar es Salaam

“Mpango huu jumuishi wa miaka mitano utakaouzinduliwa umezingatia nguzo kuu mbili, ambazo ni kuzuia na utoaji wa huduma kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia” alisema Bi. Nkinga
Alisema kuwa mpango kazi huo unatarajiwa kutoa msukumo mpya katika kuwezesha utekelezaji  majukumu ikiwemo kutetea, kushauri na kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa  kwa jamii kuhusu athari za ukatili kwa wanawake.

Kwa mujibu wa Nkinga alisema kuwa  utafiti uliofanywa na Shirika la Kuhudumia Watoto Ulimwenguni (UNICEF) wa mwaka 2015, unaonyesha kuwa Tanzania ina asilimia 3.5 ya watoto wa umri wa miaka  7 – 17 walio nje ya shule kutokana na sababu mbalimbali za ukatili.  


Alibainisha  Vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri zaidi ni pamoja na vipigo, ubakaji, ulawiti, mauaji ya vikongwe, na watu wenye ualibino, usafirishaji haramu wa binadamu, kutelekeza familia, udhalilishaji, ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.

No comments:

Post a Comment