Wednesday, 27 April 2016

SERIKALI KUAGIZA NJE SUKARI KIASI

Serikali imesema haitatoa kibali cha kuagiza mchele kutoka nje ya nchi, lakini itaagiza kiasi kidogo cha sukari ili kufidia nakisi iliyopo nchini hivi sasa kwa lengo la kuepusha mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo huku ikieleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaficha sukari ili kusubiri bei ipande.

Aidha, imewaagiza maofisa biashara nchini kote kufanya ukaguzi katika maduka ili kuhakikisha wafanyabiashara walioficha sukari ili kusubiri bei kupanda wanaitoa sukari hiyo na kuiuza mara moja.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliojadili hotuba ya Bajeti kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana.
Akizungumzia sukari, Waziri Mkuu alisema kumejitokeza kwa upungufu kidogo wa sukari nchini na serikali imeamua kuagiza kiasi hicho kutoka nje ya nchi wakati ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa nchi inapata uwezo wa kuzalisha kiwango cha sukari cha kutosha.
Alisema wakati nchi inahitaji tani 420,000 za sukari kwa mwaka, uwezo wa viwanda vya ndani umekuwa ni tani 320,000 na hivyo kufanya kuwepo kwa nakisi ya tani 100,000.
Alisema pamoja na mpango huo wa kuagiza sukari kutoka nje, serikali itakuwa macho katika kuhakikisha kuwa sukari inayoruhusiwa kuingia ni ile inayotakiwa na si zaidi, lengo likiwa ni kuvifanya viwanda vya ndani kuendelea na uzalishaji hadi kuviwezesha kufikia uwezo wa juu wa kukidhi mahitaji ya nchi.
Alisema pamoja na upungufu uliopo, serikali inazo taarifa kwamba sukari iliyopo nchini hivi sasa inafikia tani 37,000, lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakificha sukari waliyonayo ili kusubiri kupanda kwa bei kutokana na upungufu uliopo.
“Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwaagiza maofisa biashara nchini kote wafanye ukaguzi ili kuhakikisha sukari haiachwi ndani ili kusubiri bei kupanda. Ni lazima watoe sukari hiyo na wauze kwa bei elekezi ya serikali,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Bei hiyo ya serikali ndiyo itakayoruhusiwa kuwepo sokoni katika kipindi hiki cha upungufu uliopo hadi pale sukari iliyoagizwa itakapoingia nchini kutokana na kukamilika kwa taratibu zote za uagizaji wake.”
Hivi karibuni, Serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya sukari ni Sh 1,800 kwa kilo, lakini katika wiki za karibuni kumeibuka vilio vya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwamba bidhaa hiyo muhimu sasa inauzwa kati ya Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo katika maeneo yao.
Kuhusu mchele, Waziri Mkuu alisema uzalishaji wa mpunga nchini umeongezeka kwa asilimia 14 katika kipindi kinachoanzia mwaka 2009/2010 hadi mwaka 2014/2015, hatua iliyoifanya nchi kuwa na mchele wa kutosha.
Alisema kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo kunatokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha nchi inakuwa na hazina kubwa ya mazao ya nafaka zaidi.


No comments:

Post a Comment