Serikali imewataka wawekezaji wa ndani na nje kutumia
fursa zilizopo Tanzania hasa katika eneo la kuongeza thamani ya malighafi
mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Dkt. Adelhelm Meru alipokuwa akiongea na maafisa kutoka kampuni
ya nchini Ufaransa ya Endel Engie mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Maafisa wa kampuni hiyo walikuwa nchini na kufanya mazungumzo na
viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali kueleza nia yao ya kuwekeza Tanzania
na kujua fursa zilizopo nchini.
Endel ni moja ya makampuni ya Engie Group yenye mapato
yanayofikia Euro milioni 700 kwa mwaka na waajiriwa 6,000 nchini Ufaransa.
Baadhi ya shughuli za kampuni hiyo ni katika maeneo ya sayansi
za anga, viwanda vya vyakula, reli, gesi, ujenzi wa meli, nishati ya nyuklia na
viwanda vya chuma miongoni mwa vingine.
Kwa bara la Afrika, kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi za
Afrika ya Kusini, Angola na Congo DRC.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Dkt.
Meru alisema eneo la kuongeza thamani bado halijafanyiwa kazi na lina fursa
kubwa kwa watu wanaotaka kuwekeza katika viwanda vya aina hiyo.
“Kama serikali tunaweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa watu
wanawekeza kwa faida ya pande zote mbili,” alisema.
Aliwaambia maafisa wa kampuni hiyo kuwa utulivu wa kisiasa na
amani iliyopo Tanzania vinaifanya kuwa eneo bora la kuwekeza katika ukanda huu
wa Afrika.
Kampuni hiyo iko katika mchakato wa kutafuta fursa na vivutio
vya kuwekeza katika nchi za Tanzania, Kenya na Msumbiji.
Aliyataja maeneo mengine yenye fursa za kuwekeza kama madini,
Kilimo, utafutaji wa gesi na mafuta na uzalishaji nishati miongoni mwa
nyingine.
Makamu wa Rais, Maendeleo ya Kimataifa, Endel Engie, Bw. Olivier
Rousseau alisema wamevutiwa na hali ya amani, utulivu na raslimali katika eneo
hili la Afrika na hasa Tanzania.
“Tuko katika ziara ya kujifunza,” alisema.
Kwa mujibu wa afisa huyo, mwezi wa Kumi mwaka huu, wawakilishi
wa kampuni hiyo, watarudi Tanzania na mapendekezo rasmi ya maeneo watakayokuwa
wanataka kuwekeza hapa nchini.
Mbunge mstaafu wa jimbo la Mbinga Magharibi ambaye aliambatana
na wawekezaji hao, Bw. Gaudence Kayombo alisema huu ni wakati wa kuitikia kwa
vitendo azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.
Alisema uwekezaji katika maeneo hayo utasaidia kuleta
teknolojia, mitaji na uzoefu Tanzania.
Serikali imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 40 ya
ajira zote na asilimia 15 ya pato la Taifa vitokane na sekta ya viwanda.
No comments:
Post a Comment