Jeshi la Zimamoto linaendelea kuutafuta mwili wa mwanamke mmoja aliyekuwa ndani
ya gari aina ya Hiace ambalo limetumbukia bahari ya Hindi leo alfajiri mara
baada ya kuteleza kutoka kwenye kivuko kilichokuwa kinaelekea upande wa
Kigamboni.
Kwa mujibu wa msemaji
wa jeshi hilo, Briton Monyo, ajali hiyo imetokea majira ya saa 10 alfajiri na
hadi sasa wameweza kuupata mwili dereva wa gari hilo anayekadiriwa kuwa na umri
wa kati ya miaka 29-30.
Monyo anasema gari
hilo litakuwa limetitia chini kwa eneo ambalo tukio limetokea lina kina kirefu
cha maji, tope jingi na vumbi na huku jeshi likiwa halina vifaa vifaa kama
darubini ya majini.
Hata hivyo, ndugu wa
mwanamke anayetafutwa wanasema jana walitoka Mbeya kwenye msiba wa ndugu yao na
gari walilopanda la magazeti liliwaacha eneo Feri saa 10 alfajiri wakati huo
kivuko kilikuwa kimefika ndipo walipoingia na kukutana na Hiace na kukubaliana
na dereva kuwafikisha makwao mara baada ya kuvuka ng’ambo ya pili.
Hata hivyo, mwanamke
huyo alikuwa amechoka na kuingia ndani ya Hiace huku ndugu wengine tisa
wakakaa sehemu ya abiria ya kivuko.
“Lakini kabla panton
halijaanza kuondoka tulishangaa Hiace ikiserereka na kutumbukia” mmoja wa ndugu hao alisema.
No comments:
Post a Comment