Halmashauri ya Jiji la
Mwanza, imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 1 baada ya kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima tangu mwezi Januari mwaka huu na kuzielekeza fedha hizo kwenye
utengenezaji madawati 6,840.
Mkurugenzi wa Jiji la
Mwanza Adam Ngowi, amesema uamuzi wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima
ulifikiwa ili kutekeleza agizo la rais Dkt. John Magufuli linalotaka ifikapo
Juni 30 mwaka huu tatizo la madawati liwe limemalizika.
Ngowi amesema
wanafanya utengenezaji wa madawati hayo ili kupunguza pengo la madawati 11,400
ambalo linasababisha wanafunzi zaidi ya elfu thelathini kujifunza wakiwa
wamekaa chini katika halmashauri hiyo.
Aidha, amesema kuwa
katika utatuzi wa changamoto hiyo wanakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa
vifaa ikiwemo mbao hali ambayo inafanya utengenezaji wa madawati hayo kwenda
taratibu.
Kwa upande wake Mkuu
wa wilaya Nyamagana, Baraka Konisaga ametembelea kuona hali halisi ya
utengenezaji wa madawati hayo na kusema kuwa kutokana na changamto hiyo
wanaweza kufanikiwa kutatua tatizo hilo lakini sio kwa muda ambao wamepangiwa.
Konisaga amewataka
wakazi wa wilaya ya Nyamagana kila mmoja wao kwa nafasi yake achangie jitihada
hizo za kukamilisha madawati ili kuendana na muda uliopangwa na rais
kukamilisha zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment