Wednesday, 13 April 2016

RISASI ZALINDIMA MAHAKAMANI WAKATI WA KUHAKIKI NG'OMBE WILAYANI BUKOMBE MKOANI GEITA

Milio ya risasi ilirindima juzi na kuzua tafrani wakati Mahakama ya Wilaya ya Bukombe ilipohamia mahabusu ya ngo’mbe kuhakiki idadi ya mfugo iliyokamatwa ndani ya Hifadhi ya Mdendeli Muowisi Kigosi, mkoani Geita.


Inadaiwa kuwa risasi hizo zilizokuwa zikifyatuliwa na watu wasiojulikana zililenga kuwatisha waliokuwa wakiendelea na kazi ya uhakiki iliyokuwa ikisimamiwa na Hakimu Gabriel Kurwijila na kulindwa na askari 35 mahakamani wa idara ya wanyamapori. 

Katika tuko hilo, askari 10 walilazimika kujibu mapigo na kufanya eneo hilo kugeuzwa uwanja wa vita.

Baada ya askari wanyamapori na polisi kufanikiwa kuwafurusha wavamizi, walitokomea porini kabla ya kutiwa mbaroni.

Kazi hiyo iliendelea na kubaini ng’ombe wote 454 wana afya njema ndipo Hakimu Kurwijila alipoahirisha shauri hilo.

Hata hivyo, uhakiki huo ulibaini uwapo wa ng’ombe wa ziada 139 ambao kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mwasimba Hezron, inawezekana waliwafuata wenzao wanaolindwa na askari wa wanyamapori.

Kutokana na hofu ya kuvamiwa wakiwa njiani kurejea Ushirombo, Hakimu Kurwijila aliamuru askari wanyamapori na polisi kuimarisha ulinzi kuhakikisha wote walioko kwenye msafara wanafika salama.

Kesi hiyo inawakabili washtakiwa watano wanaodaiwa kukutwa wakichunga mifungo ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao leo wanaanza kujitetea na wanatarajiwa kuitwa mashahidi sita kupinga ushahidi wa upande wa mashtaka.

Washtakiwa hao ni Emanuel Wapi, Musa Manyakenda, John Wapi, Nkwabi Ngeleja na Masan Makura.


No comments:

Post a Comment