Moto mkubwa umezuka na kuteketeza vibanda vya maduka zaidi ya
150 katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera magharibi mwa
Tanzania. Moto huo ambao ulianza Jumatatu majira ya sa 2:00 usiku umeteketeza
mali na bidhaa za aina mbalimbali kama mchele, sukari, nguo, simu, pamoja na
bidhaa zingine.
Gloria Kilio ambaye alikuwa akiuza vyakula vya
nafaka, amesema stoo zake zote tatu (3) za nafaka zimeungua, “Stoo zilikuwa na
magunia ya unga, mchele na sukari lakini vyote vimeteketea,” amesema Gloria
huku akilia. Anasema wakati moto unatokea alikuwa tayari amekwisha kwenda
nyumbani na kuwaacha wafanyakazi wake wakimalizia kufunga vibanda.
Wafanyabiashara wengi wanasema walikuwa na
mikopo na wengi wao hawana bima ya mali zao. Jonasi Nyarugenda ni miongoni mwa
wafanyabiashara hao: “Moto umeteketeza stoo zangu nne zenye bidhaa mbalimbali
kama sukari, mchele, ngano na mafuta,: anasema Jonas na kuongeza, “kwakeli
ukitathimini kwa haraka siyo chini ya milioni 45 zimepotea.” Amesema kwamba
alikuwa hana bima katika mkopo wake wa milioni 20 kutoka katika benki.
Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na
ukosefu wa vifaa vya kuzima moto. Wananchi wa Karagwe imewapasa kusubiri gari
la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya uwanja wa ndege) ambako ni kilomita
120 kufika karagwe mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi
yamekwishateketea.
Diwani wa kata ya Kanoni wilaya karagwe Sabi
Rwazo amesema tukio hilo limewastua na ni tukio la kwanza la moto kuunguza soko
wilayani humo. Anasema tatizo la ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na
uhaba wa fedha. “Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa kununua
gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao yako serikali kuu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinwiro
amesema kuwa Serikali ya wilaya yake itapata gari la zima moto hivi karibuni,
“Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana na kamishna mkuu wa zima moto
ameniahidi kunipatia gari jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati
wowote gari hilo litafika wilayani Karagwe.”
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema
hawakubaliani na kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa wakitozwa
kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia huduma za zimamoto wilayani hapo
lakini wanashangaa kwa nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna
hata gari la dharura.
Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana
lakini taarifa za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda sokoni
hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo zilizokuwa katika
kibanda hicho na kusababisha moto kusambaa ghafla.
No comments:
Post a Comment