Askari Polisi wanne
kutoka wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wanachunguzwa na Jeshi la Polisi mkoani
Mwanza kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mvuvi mmoja wa kisiwa cha Kunene
wilayani Ukerewe Tabibu Kilangi kwa tuhuma za wizi wa injini za mitumbwi
zinazodaiwa kupatikana kwa njia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mvuvi huyo ambaye kwa
hivi sasa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya
rufaa Bugando jijini Mwanza,akiwa amepoteza fahamu huku akipumulia mashine kwa
siku ya tano mfululizo anadaiwa kupigwa na askari polisi wa wilaya ya Muleba
Aprili 15 mwaka huu katika kisiwa cha Siza kwa kumtuhumu kuiba injini za
mitumbwi ya wavuvi wenzake.
Baadhi ya ndugu wa
majeruhi,Yohana Wakori na Pendo Charles wakizungumzia tukio hilo wameiomba
serikali kutenda haki ikiwemo kuwachukulia hatua za kisheria askari polisi hao
wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivyo vya kikatili.
Daktari bingwa wa
kitengo cha wagonjwa mahtuti katika hospitali ya rufaa Bugando Dk. Benard
Kenemo anasema maendeleo ya kiafya ya majeruhi huyo bado hayaridhishi,huku
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Augustine Senga akizungumza na ITV kwa
njia ya simu kutokea wilayani Magu amesema jeshi la polisi bado linaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment