Mhandisi Robert Gabriel Lughumbi Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka Viongozi
wa Serikali Wilayani Chato kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani humo ili thamani ya fedha
zinazotolewa ionekane.
Akizungumza baada ya kuwasili wilayani Chato kwa mara ya kwanza tangu
kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa amesema kuwa umefika wakati watendaji kuacha
tabia ya kukaa Ofisini bali waende maeneo mbalimbali ya Wilaya ambapo
kunatekelezwa miradi ili kusimamia kwa karibu miradi inayoendelea.
" Wananchi wanatakiwa kusimamiwa ata kama fedha ni za kwao ili
kuweka miradi katika ubora unaotakiwa"Alisisitiza Lughumbi.
Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato kuhakikisha wananchi
wanakuwa katika vikundi ili vishiriki katika ujenzi na utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika vijiji kwa kuchangia michango midogo midogo kama
vile kutafuta mawe, kokoto, mchanga. Kazi kubwa ya Halmashauri ni
kuhakikisha wahandisi wanasaidia kupeleka michoro na kusimamia ujenzi wa miradi
ya Zahanati na madarasa katika vijiji husika.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato
kufuatilia ujenzi wa Bweni la wanafunzi shule ya Sekondari Jikomboe ambalo
limegharimu kiasi cha Shilingi milioni 75 ili kujiridhisha kama fedha hizo
zimetumika kama ilivyokusudiwa na kuona kama thamani yake inaonekana.
Akiwa Wilayani Chato Mheshimiwa Robert Gabriel ametembelea shule ya
Msingi Chato na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa sita na vyoo,
ujenzi wa Zahanati ya kijiji Mganza, ujenzi wa Bweni shule ya Sekondari Zakia
Meghj pamoja na Ujenzi wa Soko la dagaa Kasenda na kuagiza takukuru kufika
katika miradi hiyo ili kufuatilia matumizi ya fedha katika miradi ya Zahanati,
Bweni na madarasa.
Vilevile Mkuu wa Mkoa ametembelea ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato na
kupongeza jitihada za utekelezaji wa mradi huo zinazoendelea kwa kufikia
asilimia 63. Awali Meneja wa Tanroads Mkoa wa Geita Mhandisi Haruna Senkuku
alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa uwanja huo una Run way ya Kilometa 3 ambapo hadi
kukamilika mradi utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 39.
No comments:
Post a Comment