Naibu Waziri aliyasema
hayo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa TEDAP unaohusu upanuzi na ujenzi
wa vituo vya kupozea Umeme na njia za Umeme ambapo vituo vya kupozea Umeme
alivyovitembelea ni Mbagala, Gongo la Mboto, Kipawa na City Centre.
“Umeme ukatike pale
inapostahili tu, na endapo tatizo linatokea mfano kwenye mifumo ya Umeme ni
muhimu mkatoa taarifa mapema kwa wananchi,” alisema Subira Mgalu.
Aliongeza kuwa
ukatikaji wa Umeme unasababisha malalamiko kutoka kwa Wananchi kwani kukosekana
kwa nishati hiyo kunaathiri shughuli nyingi hasa za kimaendeleo na kiuchumi
zinazowaingizia kipato.
Aidha Naibu Waziri
aliwaagiza watendaji wa TANESCO wanaosimamia mradi huo wa TEDAP jijini Dar es
Salaam, kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika tarehe 15 Desemba, 2017.
Vilevile alieleza kuwa
utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na kwamba kukamilika kwake
kutaboresha hali ya upatikanaji wa Umeme katika jiji la Dar es Salaam.
“Nawaomba watanzania wawe na
matumaini na Serikali ya Awamu ya Tano kwani inajitahidi katika Ujenzi wa
miundombinu ya Umeme, nia ikiwa ni nishati ya Umeme kupatikana muda wote,”
alisema Naibu Waziri.
kwa upande wake,
Meneja Mradi wa Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi
Emmanuel Manirabona alisema kuwa Shirika hilo linafanya juhudi mbalimbali ili
utekelezaji wa mradi huo ukamilike ndani ya muda ulioelekezwa.
Mradi wa TEDAP
unahusisha upanuzi na ujenzi wa Vituo Vipya 19 vya kupoza Umeme wa Msongo wa kV
132/33 na kV 33/11 pamoja na ujenzi wa njia za Umeme wenye Msongo wa kV 132, kV
33 na kV 11 katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Gharama za utekelezaji
wa mradi husika ni Dola za Marekani milioni 43, ambazo zimetolewa na Benki ya
Dunia (WB) kupitia Mradi huo.
No comments:
Post a Comment