Wednesday 8 November 2017

WAKANDARASI WANAOVUNJA MIKATABA KUCHUKULIWA HATUA - NAIBU WAZIRI JUMA AWESO



Serikali imewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuwachukulia hatua wakandarasi wa maji wanaokiuka mikataba walioingia kwa kuchelewa kutekeleza miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini Mendrad Lutengano Kigola juu ya lini Serikali itamaliza kujenga mradi wa Kata ya Mtwango katika Vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na Kibao. 

 “Viijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na Kibao katika kata ya Mtwango ni miongoni mwa vijiji 12 vilivyopendekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kupatiwa huduma ya maji kupitia programu ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijjini,” alisema Awezo.

Aliendelea kwa kusema, utekelezaji wa mradi huo ulianza Juni 01, 2015 na ulitakiwa kukamilika Juni 01, 2016 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.36 ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika kijiji cha Sawala pekee ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 50.

“Hadi mwezi Novemba, 2016 mkandarasi alikuwa hajakamilisha kazi na hivyo Halmashauri kuamua kuvunja mkataba na halmashauri ilitangaza upya zabuni kwa ajili ya ukamilishaji wa kazi zilizobaki,” alifafanua Aweso.

Amesema kuwa, mkandarasi mwingine amepatikana na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba, 2017 kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.81.


Kutokana na ucheleweshaji wa mradi huo, Aweso amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwachukulia hatua wakandarasi wa maji ambao hawatekelezi miradi yao kwa muda uliopangwa ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri wananchi wanaohitaji huduma ya maji kutokana na mradi kutekelezwa kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment