Friday 10 November 2017

VP SAMIA SULUHU AWATAKA POLISI WA KIKE KUPAMBANA NA UGAIDI, UCHOCHEZI NA WIZI WA MITANDAO





Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka polisi wanawake kupambana na vitendo vya kiuhalifu ikiwemo uchochezi, wizi wa mitandao, ujangili ugaidi na utakatishaji wa fedha haramu.

Hayo ameyasema jana  Novemba 9  akifunga maadhimisho ya miaka 10 ya mtandao wa polisi wanawake yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo cha taaluma ya Polisi Kurasini.

Makamu wa Rais alisema suala la  kuwepo kwa ulinzi  ni muhimu kwa ustawi wa nchi yetu.

Alisema  kwamba  kuwepo kwa polisi wanawake kumeleta mtazamo tofauti katika jamii, watu wamekuwa wakiona polisi ni rafiki wa umma.

Aliwataka polisi kufuata sheria katika matukio yote ya unyanyasaji wa kijinsia badala ya kuwaacha kwenda kuyatatua kifamilia.

Katika vita ya unyanyasaji wa kijinsia aliwataka polisi kushirikiana kutoa elimu bila kujali jinsia kwani vita hiyo sio ya wanawake tu.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamadi Masauni aliwapongeza polisi kwa mshikamano pamoja na ujasiri waliouonyesha.

Masauni aliwahakikishia polisi kuwa kila kitakachopatikana Serikalini atahakikisha kinagawanywa kwa usawa ili kuhakikisha polisi wanafanya kazi kwa ufanisi.

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi mstaafu na mlezi wa mtandao huo  Saidi Mwema alisema alipokuwa mkuu wa jeshi hilo alipanga kubadilisha muundo wa jeshi hilo.

Alisema "nilipofanya ziara Afrika ya kusini na kuona muundo wao nilivutiwa nao sana na niliporudi  nchini  nilianzisha mfumo huo"

Naye mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa Nchini Alvaro alisema katika jeshi la Umoja wa Mataifa wapo pia polisi wanawake na wengine kutoka Tanzania.

Hivyo nawapongeza kwa ujasiri na umoja wenu kwa kudhubutu ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

Katika maadhimisho yalipambwa na vikosi mbalimbali vikiongozwa na polisi wanawake ikiwemo gwaride, kuendesha pikipiki na farasi, kikosi vya makomandoo pamoja na vyakutuliza ghasia.


No comments:

Post a Comment