Waziri mkuu Kassim
Majaliwa amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji wa matamko
yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko Serikalini.
Ametoa kauli hiyo jana
jioni (Jumanne, Novemba 7, 2017) wakati akifungua Kikao Kazi cha Baraza la
Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema ni
vema viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo
halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara
zao.
Pia amewataka viongozi
hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii
kuwa Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao
kiutendaji.
“Tunao wajibu mkubwa
kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili
kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na wananchi wote kwa
ujumla.”
Hata hivyo, Waziri
Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za
Wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
Pia amewataka wafanye
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo
inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya
Serikali.
Waziri Mkuu amesema
Mawaziri na Naibu Mawaziri wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.
Pia wasimamie
utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli wakati wa kampeni za
uchaguzi.
No comments:
Post a Comment