Thursday 23 November 2017

UCHAGUZI KATA YA SENGA MKOANI GEITA KUFANYIKA JUMAPILI HII

 
Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Geita Ndugu Ali A. Kidwaka

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Geita Ndugu Ali A. Kidwaka amewataka wananchi wa Kata ya Senga kujitokeza kwa wingi kushiriki haki yao ya kikatiba ya kumchagua diwani wao katika uchaguzi mdogo unao tarajiwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 26 Novemba 2017 kuanzia saa moja kamili asubuhi hadi saa kumi kamili jioni.

Akiongea wakati wa semina elekezi juu ya maandalizi ya  uchaguzi huo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo pamoja na makarani ametanabaisha kuwa maandalizi yote yako  tayari na limebaki jukumu lao kama wasimamizi kuwahi vituoni.

Sambamba na hilo amewataka wananchi kuwahi katika vituo vya kupigia kura na kufuata utaratibu kukamilisha uchaguzi kwa wakati na amewakumbusha jukumu la kutunza amani ya nchi ni jukumu la kila mwananchi hivyo wanapaswa kupiga kura na kurudi nyumbani kusubiria matokeo.

Ndugu Kidwaka amewataka Makarani kuwahi katika vituo vyao wanavyosimamia ili waweze kufanya maandalizi yao mapema na kuhakikisha kila mtu mwenye sifa za kupiga kura aliejiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura anatimiza haki yake.

“Ninawakumbusha na ninawasisitiza hakikisheni mnawaongoza na kuwasaidia vizuri watu wasiojiweza na wale wasiojua kusoma kupiga kura na kuangalia watu wenye mahitaji maalum muwape vipaumbele.Ali  Kidwaka

Kata ya Senga ina jumla ya vituo 29 vya kupigia kura na jumla ya wapiga kura 10,262 walioandikishwa  katika daftari la kudumu la kupigia kura.


Uchaguzi huu mdogo unafanyika kujaza nafasi ya aliyekua diwani wa kata hiyo ndugu Joel Ntinginya kukosa sifa za kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kata ya Senga baada ya kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo vya baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita kinyume na kanuni ndogo za Halmashauri na kupelekea  kutenguliwa udiwani wake.

No comments:

Post a Comment