Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
amewataka wananchi wa mkoa wa Geita kutumia fursa ya ujenzi wa Uwanja wa ndege
wa kisasa wa Geita kujikomboa kiuchumi.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo mapema leo wakati alipokuwa akiweka jiwe
la msingi la uwanja huo katika kijiji cha Nyabilezi mkoani Geita na kusisistiza
kila mwananchi kuangalia namna atakavyonufaika na uwanja huo.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba usafiri
wa anga unaimarika ili kurahisisha huduma ya usafirishaji wa abiria, hivyo
kuvutia watalii katika vivutio mbalimbali nchini”, amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa, amewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa, kutumia fursa
ya uwepo wa Uwanja wa ndege huo kukuza utalii, kilimo, ufugaji na biashara ya
madini ili kuhuisha uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Waziri Mbarawa aliongeza kuwa katika kuhakikisha Usafiri wa anga nchini
unaimarika Serikali imekarabati Viwanja vya ndege vya Mpanda, Bukoba,
Tabora na Mafia na ina mpango wa kuvijenga kwa kiwango cha kisasa viwanja 11
nchini ili kuwezesha ndege mpya za Shirika la Ndege (ATCL), kutoa huduma
katika mikoa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),
Mhandisi Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Geita ni
sehemu ya utekelezaji wa sera ya usafiri wa anga nchini ya mwaka 2003
inayooelekeza uwepo wa uwanja wa ndege wa kisasa katika kila mkoa ili
kurahisisha uchukuzi na kuchochea fursa za kibiashara na kitalii katika maeneo
mbalimabali ya nchi.
Mhandisi Mfugale, aliongeza kuwa Uwanja wa Ndege wa Geita ambao unajengwa
na Kampuni ya kikandarasi ya Mayanga ambayo ni ya mzawa kwa gharama ya zaidi ya
Shilingi Bilioni 41.
“Uwanja huu utakapokamilika utawezesha ndege kubwa aina ya Boeing 737 –
800 zenye uwezo wa kubeba abiria 100 hadi 200 kuruka na kutua, hivyo
kuongeza na kurahisisha huduma ya usafiri wa anga katika Ukanda huo”, amesema
Mhandisi Mfugale.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi, alisema wamejipanga
kutumia uwanja wa ndege wa Geita katika kukuza utalii na biashara mkoani humo
na kuahidi kuulinda uwanja huo na kutunza miundombinu yake.
Uwanja wa Ndege wa Geita wenye urefu wa Kilometa 3 na upana wa Meta 45
unatazamiwa kuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa Tatu kwa wakati mmoja pindi
utakapokamilika.
|
No comments:
Post a Comment