Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa
Sheria ya Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania ya Mwaka 2017 (The Tanzania
Telecomunications Corporation Bill, 2017) mapema leo mjini Dodoma ikiwa ni
sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuimrisha sekta ya Mawasiliano.
Akizungumza wakati akijibu hoja za Wabunge waliochangia muswada
huo Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema
kuwa kuanzishwa kwa Shirika hilo kutawanufaisha wananchi walio wengi hasa
wanaoishi maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu hali
itakayochochea kukua kwa uchumi nchini.
“Kuanzishwa kwa Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania
kutawanufaisha Watanzania wote kutokana na fursa zitakazojitokeza katika maeneo
yote ya nchi yetu zikiwemo ajira kwa kuwa Shirika hili halitabagua Watanzania
katika swala la ajira ilimradi mhusika ana sifa stahiki ” Alisisitiza Prof.
Mbarawa
Akifafanua amesema kuwa kuwepo kwa Shirika hilo kutasaidia
kuimarisha ushindani katika sekta ya Mawasiliano hapa nchini kwa kuwa Muundo wa
shirika hilo utabadilika na hata utendaji wake utajikita katika kuongeza tija
na kulinda maslahi ya Taifa.
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona kuwa shirika hilo
linafanya kazi kwa tija na kuzalisha faida hali itakayopelekea Serikali kupata
gawio kutokana na faida iliyozalishwa.
Aidha Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali imepokea maoni
ya wabunge kuhusu kuongeza mtaji wa Shirika hilo ili liweze kuongeza tija
katika kutoa huduma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment