Ajali za barabarani
zimepungua kwa asilimia 40 katika kipindi cha Julai- Septemba 2017
ikilinganishwa na kipindi hicho hicho mwaka jana.
Hayo yameelezwa leo
katika mahojiano maalum kati Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Deus Sokoni na Idara ya Habari (MAELEZO).
Sokoni amesema katika
kipindi cha Julai – Septemba mwaka 2016 ajali za barabarani zilikuwa 2639
wakati mwaka huu katika kipindi hicho hicho jumla ya ajali 1375 zimetokea
nchini.
Kwa mujibu wa Kamanda
Sokoni, idadi ya vifo pia imepungua kutoka 923 hadi 652 na ajali za pikipiki
zimepungua kutoka 653 hadi 367 ambayo ni sawa na asilimia 44.
“Kupungua kwa ajali
hizo na vifo imetokana na madereva kutii sheria bila shuruti, ushirikiano baina
ya wananchi na jeshi la polisi na elimu kwa umma ambayo tumekuwatukiitoa kwa
wadau mbalimbali, ikiwemo wanafunzi, vituo vya bodaboda na kambi za jeshi la wananchi,”
alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni amesema
makosa yanayotokana na ulevi yameongezeka kutoka 7589 hadi 7617 jambo ambalo
limeelezwa kuwa elimu bado inahitajika ili kupunguza changamoto hiyo.
Majeruhi wa ajali za
barabarani wamepungua kutoka 570 hadi 284 ambayo ni sawa na takriban asilimia
50 jambo ambalo linaonyesha mabadiliko makubwa katika kuzingatia sheria za
usalama barabarani.
Sokoni aliongeza kuwa
elimu inayotolewa kwa waendesha pikipiki imesaidia kupunguza ajali na vifo vya
waendesha pikipiki na abiria kiasi kwamba kwa mwaka 2016 katika kipindi husika
vifo vilikuwa 246 na kwa mwaka huu ni 182.
Kupungua kwa ajali,
majeruhi na vifo kumetokana na Mkakati wa Kitaifa chini ya Kikosi cha Usalama
Barabarani wa kupunguza ajali za barabarani zinasosababisha majeruhi na vifo.
Kamanda Sokoni
amewataka madereva, watembea kwa miguu, abiria na wadau wote wa usafiri
kuzingatia sheria kanununi na taratibu za usalama barabarani.
Katika kutekeleza
Mkakati huo zimefanyika operesheni za usalama barabarani katika mikoa ya
Njombe, Tanga, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Katika operesheni hizo
madereva 64 wamefungiwa leseni, wengi wao wakiwa madereva wa mabasi ya abiria
ambapo madereva 14 wamefungwa jela.
Usalama barabarani ni
jukumu la kila mtu, kwani watanzania karibu wote ni watumia barabara, hivyo
kila mmoja inabidi awe mwangalifu katika sula hilo.
Ikumbukwe Kauli Mbiu
ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ya mwaka huu ilisema Zuia ajali, Tii
Sheria, Okoa Maisha. Hivyo, madereva na waenda kwa miguu pamoja na abiria
inabidi watii sheria bila shuruti ili kuzuia ajali na kuokoa maisha.
No comments:
Post a Comment