Wednesday 8 November 2017

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU IMESEMA MFUMUKO WA BEI WASHUKA NA KUFIKIA ASILIMIA 5.1


Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Irenius Ruyobya (kushoo) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Meneja wa  Takwimu za Mazingira Bi. Ruth Minja.


Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Irenius Ruyobya (kushoo)  wakati akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba mapema hii leo jijini Dar es Salaam.


Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 5.3 ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017.

Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2017 imepungua  ikilinganishwa na mwezi septemba, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Irenius Ruyobya amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.

“ Kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Oktoba kumechangiwa na kushuka kwa gharama za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba, 2017 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba, 2016”, alisema Bw. Ruyobya.

Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na unga wa mtama umepungua kwa asilimia 2.6, samaki kwa asilimia 7.1, matunda kwa asilimia 2.7, mbogamboga kwa asilimia 7.4,maharage kwa asilimia 2.9, viazi kwa asilimia 14.4 na karanga kwa asilimia 7.8.

Ruyobya aliongeza kuwa mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya mfumuko wa bei wa mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi asilimia  5.72 toka asilimia 7.06 mwezi Septemba na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 4.8 toka asilimia 5.3 mwezi Septemba, 2017.

Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.

No comments:

Post a Comment