Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amerejesha nchi kwa wananchi na kwamba hayo ni mapinduzi ya
ajabu ambayo hayajawahi kutokea katika nchi zetu hususan Afrika.
Maneno hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayub Rioba alipofanya mahojiano na redio Uhuru
mwishoni mwa wiki iliyopita katika ofisi zao zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini
Dar-es-salaam.
Dkt.Rioba amesema Mhe. Rais ameirudisha nchi kwa
wananchi kwa kuwa anatekeleza “kile anachoambiwa na wananchi, na ahadi
alizowaahidi wakati akiwaomba kura” anaeleza Dkt. Rioba na kuongeza kuwa yeye binafsi
anamshukuru Mhe. Rais kwa “kuirudishia heshima Tanzania“.
Katika mahojiano hayo, Dkt. Rioba alieleza kuwa
tangu kushika madaraka miaka miwili sasa
Rais Magufuli amekuwa ‘busy’
kuhakikisha nchi inakaa sawa kimfumo ndio maana hajashughulika sana na safari
za kwenda nje ya nchi.
Rais anataka kutengeneza “mfumo wa kimkataba au
kibiashara na hawa mabwana wakubwa (wawekezaji toka nje) utakaowezesha kugawana
nusu kwa nusu katika kile kinachopatikana katika uendelezaji wa rasilimali zetu
badala ya mifumo ya zamani ya kukubali kila mfumo unaoletwa na nchi zilizoendelea”
alisema Dkt. Rioba.
Mkurugezi Mkuu huyo alikieleza kituo hicho cha redio
kuwa yeye binafsi anadhani kilichosababisha Kampuni ya kuchimba Dhahabu ya Barrick kumsikiliza Mhe Rais ni umakini
wa kiongozi huyo kwa “hanunuliki, hahongwi hongwi maana Afrika ina viongozi
wengi ambao wananunuliwa na kuhongwa” lakini sasa wanajua huyu ni tofauti.
Dkt. Rioba anamuona Rais Magufuli kuwa kiongozi
anayesimamia mambo yanayo wanufaisha wananchi wake na “hakimbii kimbii kwenda
huku na kule kuomba" na kuifananisha nchi yetu na zile zinazotoa misaada
katika nchi nyingine. Kwa kuwa fedha wanazozipata zinatokana na rasilimali zetu na kueendeleza nchi zao.
Mhe Magufuli alisema; “Nchi yetu ilitakiwa kuwa Donor Country, yaani nchi inayotoa
misaada kwa nchi nyingine”.
Ninachoweza kuwaambia Watanzania wenzangu miaka
miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano madarakani, hakika viongozi wetu wameonesha
nia nzuri na wanatakiwa kuunga mkono kwa hili analolifanya Rais Magufuli wakati
huu wa mpito.
Nchi yoyote inapopita katika mpito ni lazima kuna
mambo yalikuwa hayaendi sawa na mengine
yamekwenda sawa. Mpito ukitokea kuna mabadiliko yatakayojitokeza. Mfano Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipendekeza mfumo wa vyama vingi japo wananchi wengi,
bado waliutaka mfumo wa chama kimoja. Aidha
kutokana na kubadilishana uongozi hapa Tanzania, mabadiliko mengi yalijitokeza
ambayo yalikuwa mazuri na mengine sio mazuri kwa kuwa ni kipindi cha mpito.
Dkt. Rioba amesema ujio wa Rais Magufuli ulikuwa ujio
muhimu sana kwa wakati huu, kwa ajili ya kurekebisha yale yote yaliyojitokeza ambayo
hayakuwa sawa. Akitoa mfano wa mwana falsafa mmoja anayeitwa Fans Fanon wakati wa
vita vya ukombozi nchini Algeria alisema:
“Kila kizazi kinakutana na majukumu yake ya msingi ya
kutekeleza au kuyatelekeza na kusubiri matokeo yake”
Mkurugezi Mkuu huyo wa TBC alieleza kuwa kwa maoni
yake Rais Magufuli amekuwa kiongozi sahihi aliyekuja kwa wakati sahihi, ili kurekebisha
mambo kwa namna moja au nyingine ambapo hapa na pale tulijikwaa kwa sababu
tulitoka nje ya misingi iliyojengwa na Taifa letu.
Kuhusu suala la kuwa na uchumi mzuri katika nchi
Rioba amesema tafiti zinafanyika kwa mrengo wa kimagharibi zaidi ambapo,
wanahalalisha mifumo ya uchumi wanayoitaka wao. Wachumi walio wengi wanasema ili
uchumi uwe mzuri na nchi kuendelea ni lazima kuwa na Ardhi, tekinolojia,
rasilimali ziwe nyingi nk , lakini sio kweli.
Mfano nchi ya Singapore hawana rasilimali zaidi ya
bahari na samaki lakini uchumi wao ni mzuri sababu moja kubwa ni uongozi bora
ambao unasimamia matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya wananchi wa nchi
husika. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya 4 duniani kwa wingi wa
madini lakini haijaendelea, mpaka leo kuna watu wanaomiliki madini katika nchi
hiyo wako nje hivyo faida yote inayopatikana kutokana na madini hayo
inazinufaisha nchi za nje.
Jambo la msingi Rais Magufuli anataka rasilimali
zilizopo, hata kama kidogo kitumike kwa manufaa ya wananchi wanyonge wa
Tanzania. Tanzania ya Rais Magufuli
amesema hapana haya madini yanayopatikana hapa Tanzania ni lazima tugawane nusu
kwa nusu.
Dkt. Rioba anasema Rais ameonesha mfano kwa nchi
nyingine za Afrika zenye rasilimali kama zetu, kuwa hili la kugawana faida nusu
kwa nusu, hata kama hatuna tekinolojia na mitaji linawezekana.
Zipo nchi nyingi za Afrika ambazo zilitumia
rasilimali zao vibaya mfano, Siera Leoni, Liberia wakawa wanachimba almasi kwa
ajili ya kuendesha vita na kununua silaha kutoka nchi
zilizoendelea.
Afrika ifike mahali ioneshe ukomavu na kuacha
mambo ya kipumbavu kama hayo ioneshe kuwa Afrika ina watu wanaweza kufikiri na
kuweza kugawana rasilimali kama alivyofanya Rais Magufuli.
Ukiangalia nchi ya Nigeria asilimia 80 ya mafuta
yanayosafirishwa kwenda nje ni asilimia 1 tu ya mafuta hayo ndio yanarudi
Nigeria, lakini Tanzana ya Magufuli amesema hapana
Akitoa mfano Dkt Rioba alisema Baba wa Taifa mara
baada ya Uhuru wa Tanganyika, wasomi walikuwa wachache sana wasingeweza
kutosheleza katika masuala ya utaalam na kuleta maendeleo kupitia rasilimali
tulizonazo. leo hii nchi yetu imepiga
hatua kubwa sana katika suala la taaluma na elimu ambapo hatukuwa na Chuo Kikuu
hata kimoja. Leo Tanzania ina vyuo vikuu takriban 50, na wataalamu wako wengi,
tunachokosa ni Wataalamu wanaoipenda nchi yao wazalendo wenye nia ya kusukuma
gurudumu la maendeleo.
Dkt. Rioba anaeleza kuwa ni vizuri kuwa na waaalam
vijana wenye moyo wa kujituma na
uzalendo na kuwa tayari kuwa watumishi wa wananchi na kusaidia kutimiza ndoto ya Tanzania ya viwanda
na ndivyo anavyotaka Rais Magufuli.
Akizungumzia suala la kuondoa dhana ya kuwa na
matabaka ya watu katika Taifa, Rioba
amesema kwa sababu Tanzania iko katika mpito, ambapo ilitoka katika misingi ya
Ujamaa na Kujitegemea (Azimio la Arusha) na sasa ni kama kutengeneza Azimio la
Arusha jipya lakini katika muktadha wa zama za sasa. Kwa wale watanzania ambao
ni wazalendo kabisa kabisa, Dkt. Rioba anasema watakubaliana nae kuwa
anayoyafanya Rais Magufuli ni lazima aungwe mkono kwa kuwa anaipeleka nchi
panapostahili.
Dkt. Rioba katika mahojiano hayo amesema ni wakati
sasa kwa kila Mtanzania kuona uchungu kwa kila aina ya wizi wa rasilimali za
nchi na kwamba dhambi kubwa ambayo watanzania wanaweza kuifanya ni kudhani kuwa
jukumu la kulinda rasilimali za nchi ni la Rais Magufuli pekee.
“Haijawahi tokea kiongozi yeyote barani Afirika
kusema wananchi tumeibiwa mno na mbali zaidi, kutafuta suluhisho la kuibiwa
huko. Hongera Rais Magufuli jitihada zako ni ukombozi kwa rasilimali zote
Barani Afrika na mwisho wa Bara la Afrika kuwa Shamba la Bibi (akimaanisha kila
mtu anakuja kujichukulia na kundoka)” Dkt. Rioba alimazilia mahojiano hayo.
No comments:
Post a Comment