Wanafunzi watano wa
darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga wilayani Ngara mkoani Kagera
wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu
kinachoaminika kuwa bomu.
Mlipuko huo umetokea
leo Jumatano Novemba 8,2017 asubuhi wanafunzi hao walipokuwa wakiingia
darasani.
Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Misheni Rulenge, Goreti Francis amethibitisha kupokewa miili
mitatu na majeruhi 20.
Kati ya majeruhi hao,
amesema wawili walifariki wakati wakipatiwa matibabu.
“Majeruhi wana
majeraha sehemu mbalimbali za mwili, tunafanya kila jitihada kuokoa maisha
yao,”
amesema Dk Francis.
Akizungumza kwa simu
akiwa eneo la tukio, zaidi ya kilomita 50 kutoka Ngara mjini, diwani wa
Kibogora, Adronis Bulindoli amesema wanafunzi waliofariki wana umri kati ya
miaka minane na tisa.
Amesema askari polisi
kutoka Kituo Kidogo cha Kata ya Bugarama kwa kushirikiana na maofisa wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha kulinda mpaka kilichopo Bugarama
wanaendelea na uchunguzi eneo la tukio.
Juhudi za kumpata
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi na viongozi wengine wa
wilaya kuzungumzia tukio hilo zimeshindikana kwa kuwa wapo kwenye msafara wa
Rais John Magufuli aliye ziarani mkoani Kagera.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Erick Nkilamachumu amesema kuna hisia kuwa
mmoja kati ya wanafunzi hao alibeba mlipuko unaodaiwa kuwa ni bomu baada ya
kuliokota.
Kata ya Bugarama
ambako Shule ya Msingi Kihinga ipo ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi
jirani ya Burundi ambayo imekuwa na mapambano kuhusu madaraka.
No comments:
Post a Comment