Tuesday 14 November 2017

BILIONI 34.09 ZAKUSANYWA KATIKA KODI YA MAJENGO MWAKA 2016/17


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji

Serikali imesema makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yanayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 mwaka 2015/16 hadi Bilioni 34.09 kwa mwaka 2016/17.

Akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mhe. Wilfred Lwakatare leo Bungeni Mjini Dodoma aliyedai kuwa kuna athari za kuhamishwa kwa tozo ya kodi ya umiliki wa nyumba kutoka Serikali za Mitaa kwenda TRA, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesmea kuwa hatua hiyo haijaathiri mapato bali uamuzi huo umesaidia kuongeza mapato hayo.

"Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma na maendeleo kwa wananchi. Hata hivyo, hatua ya Serikali kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa TRA haikulenga kuzinyang'anya Halmashauri vyanzo vya mapato  bali kuimarisha ukusanyaji wake," alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji amesema, kumekuwepo na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi ya majengo pamoja na  matumizi ya mapato  yanayotokana na kodi hiyo.

Aidha amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ufanisi katika ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Taifa. Halmashauri zote zitapata mgawo wa fedha kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.

Ameendelea kwa kusema kuwa, makusanyo yatokanayo na kodi ya majengo yameongezeka kwa asilimia 20.6 ya makusanyo halisi yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA mwaka wa fedha 2016/17.

"Ongezeko hili la makusanyo linadhihirisha kuwa, TRA imefanya vizuri zaidi katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na Halmashauri hizo 30 katika mwaka 2015/16," alifafanua Dkt. Kijaji.

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18 (Julai - Septemba) TRA ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi cha shilingi bilioni 11.9. Hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu TRA  ilifanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 13.2 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 111.  


No comments:

Post a Comment