Wednesday, 22 November 2017

MBUNGE WA ZAMANI WA KIGOMA KUSINI DAVID KAFULILA AJIVUA UANACHAMA WA CHADEMA



Aliyekuwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amejivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai kuwa Vyama vya Upinzani haviwezi kuendesha vita dhidi ya ufisadi.
Kafulila amesema kwa sasa haoni mwanga wowote kwa vyama vya upinzani kuweza kutokomeza ufisadi ulioweka mizizi hapa nchini huku akimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi anazozionesha katika kukabiliana na ufisadi.

Tangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli achaguliwe na kukabidhiwa la jukumu la kuongoza nchi vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua sura mpya, Watuhumiwa na wahusika wa rushwa kubwa ambao walikuwa hawaguswi huko nyuma tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria, Kutokana na juhudi za kupambana na rushwa na ufisadi zinazoendelea nchini, matokeo ya tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na mashirika huru ya ndani na nje ya nchi yanaonesha kuwa kiwango cha rushwa nchini Tanzania kimeporomoka sana, Juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono na watu wote na vyama vyote vilivyojipambanua kupambana na ufisadi, Nikiwa moja ya wanasiasa vijana waliopata fursa na bahati ya kutumikia katika bunge la kumi (10) nikiwakilisha jimbo la Kigoma Kusini, siku zote nimejipambanua na kujitoa muhanga kupambana na ufisadi, Hata hivyo katika siku za karibuni na hasa tangu harakati za uchaguzi za mwaka 2015, vyama vya upinzani nchini vinaonekana kupigwa ganzi na kupoza katika juhudi zake za kupambana na ufisadi, Ghafla, ufisadi sio tena ajenda kuu ya vyama vya upinzani nchini.

Kwa sababu hii, ni wazi kuwa upinzani sio tena jukwaa salama la kuendesha vita dhidi ya ufisadi, Kwa kuwa sina tena imani na upinzani kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi, nimeamua kwa hiari na utashi wangu kujivua uanachama wa CHADEMA.“amesema Kafulila kwenye taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari.


Hata hivyo, amesema atatoa taarifa zaidi siku za usoni ni Chama gani atahamia baada ya kurudisha Kadi Chadema kwa kusema “Nitatangaza katika siku za hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zangu dhidi ya ufisadi. Nawatakia safari njema waliobaki ndani ya CHADEMA kwa kile wanachokiamini“.

No comments:

Post a Comment