Tuesday 14 November 2017

SERIKALI YATOA MAFUNZO KWA WALIMU 699 WANAOFUNDISHA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU WA AKILI


Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Willian Ole Nasha

Serikali imetoa mafunzo kwa walimu 699 wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji ili kukidhi mahitaji ya ujifunzaji kwa wanafunzi hao.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Willian Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Mariam Kisangi juu ya mpango wa Serikali katika kuboresha vitengo vya Elimu kwa watoto wenye wenye ulemavu wa viungo na ubongo.

"Serikali inatambua uwepo wa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji na jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata fursa ya elimu kama watoto wengine," alifafanua Ole Nasha.

Aliendelea kwa kusema, takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji 11,386 katika ngazi ya elimu ya awali na msingi ambapo wanafunzi wenye ulemavu wa viungo 8,115 wanaosoma ngazi ya Elimu ya awali, msingi na sekondari.

Ole Nasha amesema, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kupanua fursa za upatikanaji wa elimu na kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu nchini.

Aidha amesema, licha ya kutoa mafunzo kwa walimu hao, Serikali imeanzisha na kuimarisha vitengo 349 vinavyopokea wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji nchini pamoja na kufanya mapitio ya mwongozo wa ujenzi wa majengo  ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.  
  
"Mwongozo huu utazingatia mahitaji maalum ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo wawapo shuleni," alifafanua Ole Nasha.

Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inakamilisha uandaaji na mwongozo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji ambao utasambazwa katika vitengo vyote 349 vinavyopokea wanafunzi  hao.

Mwongozo huo unalengo la kupanua uelewa wa walimu juu ya mbinu za kufundishia, matumizi ya vifaa pamoja na saikolojia ya walimu juu ya mbinu za kufundishia, matumizi ya vifaa pamoja na saikolojia ya kufundishia wanafunzi  hao kwa ubora zaidi.

Katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali imetenga Shilingi 3.5 kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, akili na wenye usonji.
 

No comments:

Post a Comment