Serikali imesema
katika mwaka wa fedha 2017/2018 Jeshi la Polisi limetenga jumla ya
shilingi Bilion 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya Wakandarasi
waliotekeleza miradi mbalimbali ya Jeshi hilo.
Hayo yamesemwa na
Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni leo Mjini Dodoma
wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Ayoub
kuhusu madai ya Mkandarasi aliyejenga vituo vya Polisi Mkokotoni Unguja na
Madungu.
Mhandisi Masauni
ameeleza kuwa fedha hizo zilizotengwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Kituo cha
Polisi Mkokotoni ambao umetengewa jumla ya shilingi Milioni 200
ikiwa ni sehemu anayodai mkandarasi huyo.
“Serikali inatambua madeni ya
Wakandarasi wote ikiwemo Albatna Builing Contractor na ina nia ya dhati ya
kuyalipa madeni yote ya Wakandarasi na washauri elekezi waliohusika katika
miradi mbalimbali ikiwemo miradi iliyohusisha Jeshi la Polisi,” amefafanua Mhandisi Masauni.
Wakati huohuo Mhandisi
Masauni amesema kuwa, Serikali imekuwa na mpango wa kupeleka fedha za Maendeleo
kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa samani katika Magereza nchini ikiwemo
Gereza la Karanga.
“Katika kukabiliana na changamoto
hiyo, Serikali inatekeleza mpango wa muda mrefu wa kuyaboresha majengo hayo kwa
kuyafanyia ukarabati mkubwa unaolenga kuyaimarisha, kuyaboresha na kuyafanyia
upanuzi,” aliongeza Mhandisi
Masauni.
Aidha amesema kuwa,
kutokana na ufinyu wa bajeti fedha hizo zimekuwa zikitolewa kwa awamu katika
Magereza mbalimbali nchini ili kufanikisha uboreshaji wa majengo hayo.
No comments:
Post a Comment