Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe amemshukuru Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini
Bibi. Wang Ke kwa kuipatia wizara vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 133.
“Nashukuru sana Balozi kwa kutupatia msaada wa
vitendea kazi na tunaahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi
mbili kwa manufaa ya taifa na watu wake” amesema Mhe.Dkt.
Mwakyembe.
Aidha Waziri Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa tayari
kumekuwa na juhudi za wazi zinafofanywa na Ubalozi huo kwa kutoa mafunzo ya
kubadilishana utaalam kati ya Tanzania na Jamhuri ya watu wa china kupitia
sekta za filamu, habari,michezo na utamaduni.
Pia, Dkt. Mwakyembe alimueleza Balozi huyo kuwa
Tanzania imepata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa programu ya Urithi wa Ukombozi wa
Bara la Afrika wenye lengo ya kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kuikomboa
Afrika ili kuwa na historia nzuri kwa kizazi kijacho.
“Tayari tumeanza maandalizi ya kuhifadhi historia ya
wapigania uhuru ukizingatia Tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
nchi za Bara la Afrika zinakuwa huru, hii ni hatua kubwa kwetu katika
kuimarisha mahusiano baina ya nchi zetu ” amesema Mhe. Dkt. Mwakyembe.
Naye Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Bibi.
Wang Ke ameeleza kufurahishwa na ushirikiano ulipo baina ya nchi hizo mbili
ikiwemo kujifunza tamaduni za China.
“Nimefurahi kuona idadi kubwa ya watanzania
wanaojifunza utamaduni wetu kupitia Chuo kikuu cha Dar es Salaama na Chuo kikuu
cha Dodoma, ni hatua nzuri na ya msingi katika kuimarisha mahusiano ya nchi
zetu” amesema Balozi Wang Ke.
Tanzania na
Jamhuri ya Watu wa China wamekuwa na ushirikiano wa karibu katika kuleta
maendeleo tangu mwaka 1960 ambapo walishirikiana katika ujenzi wa reli ya
TAZARA na sasa uhusiano huo umezidi kuimarishwa kupitia sekta za habari,filamu,
sanaa na utamaduni.
No comments:
Post a Comment