Wednesday 8 November 2017

MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO AJIFUNGUA CHOONI MKOANI GEITA




Mwanafunzi  mwenye umri wa miaka 13 ambaye anasoma darasa la tano Shule ya Msingi Ibondo, Kata ya Rudete, Wilayani Geita, (Jina tunaliifadhi) amejifungua  kabla ya wakati katika choo cha shule baada ya kupata uchungu wa ghafla.
Hali hiyo ilizua taharuki miongoni mwa wanafunzi na walimu shuleni hapo ambapo mtoto huyo alipokimbilia chooni baada ya kujisikia haja kubwa na badala yake alitoka mtoto wa umri wa kati ya miezi 4hadi 5.

Akisimulia mkasa huo, Mwanafunzi huyo alisema kuwa muhusika wa ujauzito huo ni kijana mkaazi wa kijiji hicho ajulikanaye kama Laurent Ngasa, alisema siku ya tukio  alikuwa hayupo vizuri kwani  alipata maumivu ya kichwa,na baadaye wakati masomo yakiendelea alijisikia kupata haja kubwa na alipokwenda chooni ndipo hali hiyo ilipomtokea.

 “Nilipofika chooni nilisikia kitu kinatoka kumbe ni mtoto nilipatwa na hofu nikakimbilia nje nyuma ya moja ya madarasa nikachuchumaa na ndipo kikatoka tena kitu kingine sasa hapo ndipo wanafunzi wenzangu wakakimbila kuwaambia waalimu,”alisema Mwanafunzi huyo.

Aliwezaje kuhudhuria masomo kwa miezi kwa miezi hiyo yote bila kugundulika.

Baada ya kuhojiwa kuwa aliwezaje kuficha ujauzito huo bila wazazi na walimu kumtambua kuwa ni mjamzito,  alisema walimu na wanafunzi wenzake walikuwa wakimuuliza kuwa kwa nini ana tumbo kubwa lakini hakuna aliyehisi kuwa ni mjamzito.

“Kuna siku moja mwalimu mmoja aliniita mara tu baada ya kupata chakula cha mchana, akaniuliza mbona tumbo lako kubwa sana, nikamjibu kuwa nilikula wali mwingi,”alisema.

Akizungumzia kuhusu hali ya mtoto huyo, baba wa mwanafunzi huyo, Wiliam Bukwimba, alikanusha kuwa na taarifa wala kuhisi kuwa mtoto wake ni mjamzito katika kipindi chote cha ujauzito huo.

“Kusema kweli sikuwahi kumgundua huyu mwanangu kuwa ana ujauzito na kila siku alikuwa akihudhuria masomo yake kama kawaida,”alisema.

Naye rafiki wa Mwanafunzi huyo, aliyejitambulisha kama Rebeka Ades, ambaye wanakaa dawati moja, naye pia alikanusha kujua wala kuhisi kuwa rafiki yake huyo ana ujauzito.

Alisema kuna siku walikuwa pamoja wakipata chakula cha mchana ambapo mwalimu alimwita na kumuuliza kwa nini amekuwa na tumbo kubwa sana na akamjibu kuwa ameshiba sana.

“Hata wakati wa kipindi cha michezo,  alikuwa anatabia ya kukaa pembeni huku akionekana na mawazo mengi tulikuwa tukimcheka sana kuhusu tumbo lake lakini hatukujua kuwa ni mimba,”alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Rudete, Sebastian Benedicto alisema tukio hilo ni la kusikitisha sana na kwamba ni lazima muhusika wa ujauzito huo achukuliwe hatua kali za kisheria.

Aidha, alisema alipata taarifa ya tukio hilo wakati wa ziara yake kwenye kata hiyo ambapo alitembelea maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii zikiwemo shule, zahanati na kuangalia changamoto zilizopo katani mwake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika zahanati ya kijiji hicho, wahudumu walifanikiwa kumfanyia vipimo na kujidhihirisha kuwa  alikuwa na ujauzito.
.

Akifafanua juu ya hali ya usalama wa mtoto huyo, muhudumu wa Zahanati ya Ibondo, Aloyce Aron, alisema walimpokea mtoto huyo saa 7.30 mchana ambapo vipimo vilionyesha kuwa alikuwa na mimba ya umri kati ya miezi 4-5.

No comments:

Post a Comment