Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye
akizungumza na vijana wa Jogging club Mjini Dodoma mara baada ya kufanya
mazoezi ya pamoja yenye nia ya kuimarisha afya na kuendeleza michezo nchini
yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma leo March 1, 2017.
Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amewahakikishia wapenzi wa
Mpira Mjini Dodoma kuwa timu za Mpira Mkoani humo zitashiriki Ligi Kuu ili
kuwapa raha ya Ligi hiyo mashabiki wa mpira na michezo kwa ujumla.
Amezungumza hayo mara
baada ya kukutana na kufanya mazoezi na Vijana kutoka Jogging Club mbalimbali
Mjini Dodoma ikiwa ni ishara rasmi ya Wizara yake kuhamia katika Makao Makuu ya
nchi.
Mhe. Nape Nnauye
amesema kuwa haitawezekana Serikali ikahamia Dodoma na kusiwe na timu
inayoshiriki Ligi kuu ya Mpira wa Miguu Tanzania Bara hivyo yeye kama Waziri
anayehusika na Michezo kwa kushirikiana na wadau wa Michezo atahakikisha Timu
zinafanya vizuri na kushiriki Ligi hiyo.
“Haiwezekani Rais akawa
hapa na Makamu wa Rais na Mawaziri tukakosa ladha na furaha ya Ligi kuu hapa
Dodoma nitahakikisha timu za hapa zinashiriki Ligi kuu”alisistiza Mhe. Nnauye.
Kwa upande wake Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu kazi Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amewapongeza
vijana wa Jogging club na wakazi wa Dodoma kwa kushiriki michezo na kuhimiza
kujituma zaidi kwa timu za michezo hasa mpira wa miguu ili kushiriki Ligi kuu
Tanzania Bara.
Naye Katibu Mkuu
Wizara wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
amewaomba wakazi wa Dodoma kufanya michezo kuwa ni Utamaduni wao wa kila siku
ili kujenga Taifa la wapenda michezo kwa nia ya kuimarisha afya na kuendeleza
michezo nchini.
Aidha Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Michezo Nchini Bw. Omary Singo amewahakikishia wakazi na wapenzi
wa Michezo ushirikiano katika kuendeleza na kukuza michezo hasa katika makao
makuu ya nchi Dodoma.
No comments:
Post a Comment