Mauaji ya Watanzania kwa njia ya kuchinjwa
yanaendelea kushika kasi baada ya usiku wa kuamkia jana wakazi wanane wa
kitongoji cha Kibatini, kata ya Mzizima jijini Tanga kukusanywa kwa mwenyekiti
wa kitongoji na kisha kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.
Watu hao ambao
inadaiwa kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana kwa kuvunja milango
ya nyumba tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala na kuwachinja kisha kuiba
biskuti, mchele na sukari na kutokomea navyo kusikojulikana.
Wauaji hao inadaiwa
wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani ya mapango ya
Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa ya uvamizi ili kupora vyakula na
kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo katika duka kuu la
Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Mmoja wa shuhuda wa
mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa Kibatini, katika mahojiano
jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha mauaji ya wenzao ni kulipiza kisasi.
“Wiki iliyopita majira ya saa tano asubuhi
hapa tulikamata vijana saba kati ya wanane wenye umri wa kama miaka 13 ambao
walikuwa wakiranda randa hapa kitongojini ili kutafuta namna ya kuvuka mto
kwenda ng’ambo ya pili na ndipo mmoja wao alipotutoroka,” alieleza Leonard na kuongeza:
“Watoto hao tulipowaweka chini ya ulinzi na
kuwahoji tukaanza kuwatilia shaka hivyo mwenyekiti aliamua kuripoti Polisi na
ndipo hao wakawachukua kwa ajili ya mahojiano na hatukufuatilia tena kujua
kwamba waliachiwa au la kwa sababu hao watoto sio wenyeji wala wakazi wa eneo hili.”
Aliongeza kwamba
wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya kitongoji kabla
ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji kuhusu mahali walipopelekwa
watoto saba.
Diwani wa Kata ya
Mzizima, Fredrick Charles alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha
kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mleni
uliopo kwenye kata hiyo.
“Hali ya usalama hapa kwetu Mzizima si shwari
kwa sababu wananchi wangu wa Kibatini wamevamiwa na kuchinjwa usiku wa kuamkia
jana majira ya saa sita usiku,” alisema Chiluba.
Naye Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Mleni kilichopo kitongoji hicho, Shabani Amani alisema
wamepatwa na hofu kubwa kuhusu matukio hayo.
“Tunadhani kuna mapungufu katika suala la
ulinzi hapa kwa sababu baada ya kutokea matukio kadhaa eneo letu hasa baada ya
kudaiwa kwamba mapango waliyojificha wahalifu yako hapa jirani na kwetu
kikosikazi cha mchanganyiko wa askari polisi na wa JWTZ wanafanya doria kwa saa
24 lakini tunashangaa kwa nini matukio yanaendelea,”alisema Amani.
Kwa upande wake,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha mauaji hayo. “Mei
30, mwaka huu majambazi waliokuwa na visu na mapanga walivamia kaya tatu na
kuua wananchi majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Paul.
Aliwataja waliouawa ni
Issa Hussein (50) ambaye ni mmiliki wa kaya hiyo pamoja na kuibwa biskuti,
mchele na sukari katika duka dogo. Wa kaya nyingine ni Mkola Hussein (40) na
Hamis Issa (20), Hamis Issa (20) na aliyemtaja kwa jina la Mikidadi (70).
Kamanda aliwataja
marehemu wengine ni Mahamud (35) ambaye ni mkwe wa Mikidadi, Issa Ramadhani
(25), Kadir (25) na Salum ambao ni wachunga ng’ombe kijijini humo.
Hata hivyo, mashuhuda
wa tukio hilo akiwemo mke wa marehemu Mkola aitwaye Aisha Saidi, alisema walipofika
nyumbani hapo waligonga mlango na kumtoa nje Mkola na kuondoka naye.
“Nimeachwa mjane na watoto sita... Baada ya
hao watu kuingia walimkamata Mkola na kumdai aeleze kwamba watoto wao saba
wamepelekwa wapi na alipojibu sijui wakamtoa nje na kumkusanya pamoja na
wanakijiji hao wengine na kuwachinja eti tu kwa sababu hawakutaja mahali
walipopelekwa watoto,” alisema
Aisha.
Katika hatua nyingine,
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa kupokea taarifa
za vitendo vya mauaji ya kikatili vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali
nchini.
“Wimbi hili la matukio ya vitendo vya mauaji
na ukatili uliojitokeza kwa kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya kuishi
ambayo ndio msingi wa haki zote za binadamu kwa ujumla wake.
"Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
inalaani vikali mauaji haya yote na matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu
yanapotokea popote nchini,” ilieleza taarifa
ya Mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga.
Tume iliishauri
serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa
wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani jukumu la kwanza la kuhakikisha
usalama wa wananchi ni jukumu la serikali.
Jeshi la Polisi
lihakikishe watu wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria
ichukue mkondo wake, ilieleza.
No comments:
Post a Comment