Wadau wa elimu Mkoani
na wilayani Geita,wameombwa kujitokeza kuchangia suala la elimu, ikiwa ni
pamoja na kutoa madawati kwaajili ya kutengeneza mazingira bora ya kupatia
elimu kwa wanafunzi.
Rai hiyo imetolewa na
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita, Ally Kidwaka,wakati
alipokabidhiwa madawati 240 yenye thamani ya milioni 12 na laki 6 kutoka kwa
mjasiliamali Evarist Gervas, na kusema kuwa ni vyema kuhakikisha kuwa
kila mdau anashiriki vyema katika kuchangia madawati ili kutatua changamoto ambazo
zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kutokana na uhaba wa madawati.
Kwa upande mwingine
Afisa elimu wilayani hapa, Deus Seif amesema kuwa upungufu wa
madawati kwa wilaya ya Geita ni mkubwa hali ambayo inawalazimu watoto
wengi kusoma wakiwa wamekaa chini.
Aidha kwa upande wake
Evarist Gervas, amewaomba wafanyabiashara na wananchi wengine kwa ujumla
kujitokeza kuunga juhudi za kusaidia elimu katika maeneo wanayoishi huku
akionesha mfano kwa kuwa mchangiaji mzuri katika masuala ya elimu tangu mwaka
2013 alipotoa madawati na kujenga madarasa.
Diwani wa Kata ya
Nyarugusu, Swalehe Juma amemshukuru mfanyabiashara huyo kwa kuonyesha
moyo wa upendo kwa kujitolea kuchangia na kuunga mkono suala la elimu.
No comments:
Post a Comment