Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amewataka Watanzania, viongozi wa dini zote kushirikiana kwa pamoja
kupiga vita matukio maovu ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali
nchini.
Amesema anatarajia
hali ya amani, usalama na utulivu inaendelea kuwepo nchini, hivyo wananchi
hawana budi kushirikiana na kushikamana na Serikali katika kuhakikisha matendo
maovu hayatokei katika maeneo yao.
Waziri Mkuu ameyasema
hayo jana (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati alipowasili mkoani Geita kwa
ajili ya kuhudhuria ibada ya kuwekwa wakfu Padre Flavian Kassala kuwa Askofu
mpya wa Jimbo Katoliki Geita.
“Mfano tukio la Mwanza watu wanavaa kanzu na
wanaingia msikitini na kukuta wenzao wanafanya ibada kisha wakawachinja, hii
haiwezekani kwa binadamu wa kawaida hivyo tushirikiane katika kupiga vita
matendo haya,” alisisitiza.
Hivi karibuni jumla ya
watu 15 waliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga katika mikoa ya Mwanza,Tanga, Dar
es Salaam na Mara.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga amesema vitendo vya
watu kuuawa kwa kukatwa mapanga vimepungua baada ya kuanzisha kampeni maalumu
ya kukemea mauaji hayo.
Alisema katika kampeni
hiyo wameamua kuwatumia walimu, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wauguzi
ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina
na badala yake wajikite katika masuala ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment