Gesi ya helium ya takribani futi za ujazo bilioni 54 inayoelezwa kuwa adimu
duniani, imegundulika nchini Tanzania na kuiweka nchi kuwa miongoni mwa mataifa
machache yenye madini mengi na muhimu.
Wagunduzi wa gesi hiyo
ni watafiti kutoka vyuo vikuu viwili nchini Uingereza vya Oxford na Durham kwa
kushirikiana na wataalamu wa madini kutoka nchini Norway.
Watafiti hao
wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi hiyo ya barafu, kama
inavyofahamika katika eneo la Bonde la Ufa nchini.
Taarifa za waandishi
wa habari nchini Japan, zimeeleza kuwa watafiti hao wamesema kuwa uhaba wa gesi
hiyo duniani ulikuwa umesababisha taharuki haswa kwa madaktari, ambao wanatumia
gesi hiyo adimu kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama ‘MRI scanners’.
Pia hutumia katika
mitambo ya kinyuklia na katika sekta nyingine nyingi za kiteknolojia.
Wiki iliyopita, Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akijibu swali bungeni
mjini Dodoma alisema madini yanayotumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia
vifaa vya matibabu kama MRI na NMR, yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.
Hata hivyo,
hakufafanua zaidi kiasi cha madini hayo na namna nchi itakavyonufaika na
ugunduzi huo. Hata alipotafutwa jana, simu yake ya mkononi ilipokewa na
msaidizi wake na kueleza kuwa waziri yuko kikaoni. Madini aina ya helium
yanatumika kwa ajili ya mitambo na pia kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na
NMR.
Kabla ugunduzi huo,
watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo ifikapo mwaka wa 2035.
Mnamo mwaka 2010,
mwanasayansi ambaye alikuwa mshindi ya Tuzo la Nobel, Robert Richardson
alitabiri kumalizika kwa gesi hiyo katika kipindi kifupi. Ukosefu huo ulikuwa
umesababisha wataalamu, kuhimiza kutungwa kwa sheria itakayopunguza matumizi
yake katika bidhaa zisizo za dharura.
Mtaalamu kutoka Chuo
Kikuu cha Oxford, Chris Ballentine alisema gesi hiyo iliyopatikana nchini
inaweza kujaza silinda za gesi milioni 1.2 za mashine za MRI.
No comments:
Post a Comment