Taasisi ya Twaweza imetoa
matokeo ya utafiti wake, ambapo imebainika kuwa asilimia 79 ya
Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja
(Live ) ya Bunge.
Katika maoni yao, wananchi hao wamedai kuwa ni haki yao ya
msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao mbalimbali vya Bunge.
Utafiti wa taasisi hiyo umefanywa katika maeneo tofauti ya
Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.
Akitoa taarifa ya matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar e
Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema suala hilo
limeonekana kutokuungwa mkono na wananchi wengi.
“Asilimia kubwa ya
Watanzania wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja
ya Bunge. Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu wengi na maamuzi haya ya
Serikali yakionekana kutoungwa mkono.
“Katika utafiti huu
wananchi nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa
mkono kwa hatua hiyo,” alisema
Eiyakuze.
Akizungumzia sababu walizozitoa wananchi wanaotaka
matangazo ya Bunge yarushwe moja kwa moja, Eiyakuze alisema asilimia 46
walisema yanawafanya waweze kufuatilia utendaji wa wabunge waliowachagua kwa
kuwa huko ndio walikowatuma.
“Asilimia 44 wanasema
ni muhimu kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu kinachoendelea bungeni,
asilimia 29 wanasema matangazo ya moja kwa moja yalikuwa yanaaminika zaidi kwa
watazamaji na wasikilizaji kuona na kusikia wenyewe kile kinachoendelea
tofauti na mfumo wa kurekodi ambapo kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.
“Asilimia 16 walidai
kuwa inafursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya kuzisoma kwenye
magazeti huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia wanachi kufuatilia
mijadala ya Bunge kwa wakati”, alisema
Eiyakuze.
Pamoja na hali hiyo mkurugenzi huyo alisema katika utafiti huo
asilimia 92 ya wananchi walisema kuna umuhimu wa vipindi vya Bunge
kurushwa moja kwa moja kupitia Luninga na redio bila kujali gharama
zilizoelezwa kuwa ndio chanzo cha kufikia uamuzi huo.
“Asilimia 88 walisema
vipindi vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama ukilinganisha na asilimia
12 ambao waliona ni muhimu suala la bajeti likazingatiwa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema asilimia 80 wanaona matangazo ya moja
kwa moja kutoka bungeni ni muhimu kama yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha
hizo zitumike kwenye huduma nyinge za jamii.
Akizungumzia suala la vyombo vya habari vya binafsi kuruhusiwa
kurusha matangazo hayo, Eiyakuze alisema wananchi wanaunga mkono vyombo
hivyo kuruhusiwa iwapo Serikali imeshindwa kumudu gharama.
Utafiti huo pia umeonesha Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi
kuangalia matangazo ya moja kwa moja kupitia Luninga na sita kati ya kumi
wamesikiliza kupitia redio.
Aidha utafiti huo umeonyesha zaidi ya nusu ya wananchi walosema
wameangalia au kusikiliza vipindi vya Bunge wamefanya hivyo ndani ya miezi
miwili iliyopita.
Hali ilivyokuwa
Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye, alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya Serikali
kusitisha matangazo hayo kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Miongoni mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama
kubwa ya Sh bilioni 4.2 zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya
moja kwa moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia Bunge badala ya
kuendelea na kazi ofisini.
Hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa
bungeni huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, (ACT-Wazalendo) akilitaka
Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya Serikali.
Siku chache baadaye kilio hicho cha ukosefu wa fedha za kuonesha
matangazo hayo ya moja kwa moja ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa
kilipata ufumbuzi.
Hatua hiyo iliyokana na uamuzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari
nchini (TMF), kujitokeza hadharani na kueleza kwamba upo tayari kutoa fedha
zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari kupitia TBC
haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.
Endapo Serikali itakubali ombi hilo, wananchi wataendelea
kunufaika na vikao vya moja kwa moja vya Bunge tofauti na pendekezo la serikali
la kunakili baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku.
No comments:
Post a Comment