Serikali ya Tanzania imepitisha bajeti ya shilingi trilion 29.5
kwa kupigiwa kura huku wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba
midomo yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na
Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu
Spika huyo
Katika vikao vya Bunge la 11, wabunge wa vyama vya upinzani
wamekuwa wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku 23 sasa kwa madai ya
kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa Bunge Dkt.Ackson
Tulia.
Wakichangia bajeti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini Prof
Sospeter Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Charles
Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika Bajeti
hiyo ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha katika ofisi ya mkaguzi wa serikali
CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na kuachana na mpango wa kuanza kuwakata
kodi wabunge katika mafao ya kiinua mgongo ya Wabunge, Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema msimamo wa serikali upo pale pale.
Kuhusiana na makato ya kodi kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango
amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata kodi hiyo kwa viongozi wote wa
kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na
Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi nchini.
Baadaye jioni wabunge walipiga kura mmoja mmoja kupitisha bajeti
hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo bungeni walipitisha bajeti hiyo kwa
kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu "Ndiyo" akimaanisha
anaipitisha bajeti hiyo.
Mapema Asubuhi mara baada ya dua, wabunge wa upinzani waliziba
midomo yao kwa karatasi na Plasta na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni
ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.
Mbunge wa Vunjo Kupitia chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. James
Mbatia kwa niaba ya wabunge hao alisema hawataacha kulalamikia ukiukwaji wa
sheria unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.
No comments:
Post a Comment