Mbunge wa Viti Maalumu
(CCM), Fakharia Khamis amehoji bungeni adhabu gani askari anapewa ikiwa
atashindwa kutoa saluti kwa mbunge.
Katika swali la
nyongeza mbunge huyo alitaka kujua maana ya saluti kwa askari ni nini, na
viongozi gani wa uraiani wanaotakiwa kupigiwa saluti katika mhimili wa Bunge,
Serikali na Mahakama.
Akijibu swali la
mbunge huyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha kwa
niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema Serikali imetangaza adhabu ya
kuwakata mishahara na adhabu nyingine, askari polisi wote nchini ambao
hawatawapigia saluti wabunge wa Bunge la Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Ole Nasha alisema
kumpigia saluti mbunge ni jambo la lazima kwa askari kwa kuwa lipo kwenye moja
ya masharti yao, hivyo kutokufanya hivyo ni kushindwa kutii kiapo cha uaminifu
wao.
“Askari asipotoa
saluti unatakiwa kumripoti kwa kiongozi wake ambapo atapewa adhabu ikiwamo
kukatwa mshahara, kupigishwa paredi, kufanya usafi katika maeneo ya vituo na
adhabu nyingine nyingi zinazofanana na hizo,” alisema Ole Nasha.
Alisema saluti ni
salamu ya kijeshi ambayo hutolewa na askari kwa mujibu wa kanuni za kudumu za
utendaji za jeshi la polisi (Police General Orders –PGO No 102).
Naibu Waziri alisema
sheria hiyo imewataja askari wa vyeo vyote kuwa wanatakiwa kupiga saluti kwa
Rais wa Jamhuri na Rais wa Zanzibar, Makamu wa Rais na Makamu wawili wote wa
Zanzibar, majaji wakuu wa Muungano na Zanzibar.
Wengine ni Spika wa
Muungano na Zanzibar, mawaziri wote wa Jamhuri na Zanzibar, makatibu wa Bunge
na Baraza la Wawakilishi, wabunge wa muungano na wawakilishi wanapokuwa kwenye
maeneo yao, wakuu wa mikoa, majaji wanapokuwa kwenye maeneo yao na kwa nafasi
zingine ni wakuu wa wilaya na mahakimu kwenye maeneo yao.
No comments:
Post a Comment