Friday, 24 June 2016

WAZIRI MKUUU KASSIM MAJALIWA KUWA MGENI RASMI SHINDANO LA KUHIFADHI QURAN



Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran, Shekh Othman Kaporo (katikati) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu shindano la kimataifa la kuhifadhi Quran litakalohitimishwa Juni 26 mwaka huu Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkuu wa Utendaji wa Jumuiya hiyo Ally Sindo na kulia ni Katibu wa Jumuiya hiyo, Mohamed Ali.



Mtoto mwenye umri wa miaka 8, Khalid Abudhar mshiriki wa shindano la kimataifa la kuhifadhi Quran  kutoka Tajikstan akisoma Quran kwa kichwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.



Baadhi ya washiriki kutoka nchi mbalimbali watakaoshiriki katika shindano la kimataifa la kuhifadhi Quran litakalofanyika Jijini Dar es Salaam wakimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran, Shekh Othman Kaporo (hayupo pichani). 



Mshiriki wa shindano la kimataifa la kuhifadhi Quran kutoka Bangladesh Ahmed Abdallah akisoma Quran kwa kichwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha shindano la kuhifadhi Quran (TAHFIIDHI) litakalofanyika Juni 26 mwaka 2016.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran Tanzania, Shekh. Othman Kaporo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu shindano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee kuanzia saa mbili asubuhi.

“Tunaandaa mashindano ya Quran kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuhifadhi Quran pamoja na kuhamasisha vijana na watu wazima kushikamana na masomo halisi ya kuhifadhi na kuifahamu Quran hivyo,kuwafanya waislaam kuwa watu wema na wenye maadili yaliyotukuka”, alisema Shekh. Kaporo.

Shekh. Kaporo amefafanua kuwa shindano la kimataifa litashindanisha jumla ya washiriki kutoka nchi 16 zikiwemo Sudan, Kuwait, Bangladesh, Urusi, Tajikstan, Afrika Kusini, Tanzania, Nigeria, Uganda, Burundi, Kenya, Yemen, Dubai, Ufilipino, India na Malawi ambapo kila nchi itatoa mshiriki mmoja.

Aidha shindano hilo litasimamiwa na jopo la majaji 7 kutoka nchi za Sudan, Kuwait, Bangaladesh, Urusi, Tajikstan, Afrika Kusini na Uingereza.


Shindano la kuhifadhi Quran kitaifa lilifanyika mnamo tarehe 7 na 8 mwaka huu na washindi wake watashiriki shindano la kimataifa litakalofanyika kwa siku tatu kuanzia Juni 23 mwaka huu na mshindi anatarajiwa kupewa zawadi ya fedha zaidi ya dola 5000 za kimarekani.


No comments:

Post a Comment