Sakata Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limezidi kupanuka baada ya wanafunzi
waliorudishwa nyumbani kupinga kuitwa vilaza.
Jana wawakilishi wa
wanafunzi hao ambao waliambatana na viongozi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania
(TSNP), walisema wanapinga pia hatua ya kutimuliwa chuoni.
Akizungumza kwa niaba
ya wanafunzi wenzake, Gibson Johnson alisema wanasikitika kuona wanavyozushiwa
tuhuma mbalimbali kuhusiana na wao kujiunga na chuo hicho.
Alisema wamekuwa
wakijiuliza sababu za Serikali zinazotaka kuhalalisha kutimuliwa kwao chuoni
kuwa hawakuwa na sifa, jambo ambalo si la kweli.
“Siyo kweli kwamba sisi ni vilaza
(wanafunzi wasiofanya vizuri darasani) na waliofeli na kupata daraja sifuri.
“Sisi ni wanafunzi tuliofaulu kwa viwango vilivyohitajika kwa daraja la
kwanza hadi la tatu na tulipangiwa shule za kuendelea na masomo ya kidato cha
tano na sita, lakini tulibadili na kuamua kujiunga Udom, hivyo tunaomba
Serikali itumie busara zake.
“Hatuwezi kwenda kusoma kidato cha tano na
sita kwa kuwa tumepoteza muda wetu.”
Alisema wanamshauri
Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Rais John Magufuli kutumia busara
kuwarudisha chuoni kumalizia masomo yao.
Katibu Mkuu wa TSNP,
Alphonce Lusako aliitaka Serikali ichukukue hatua kwa waliohusika
kudahili wanafunzi wasio na vigezo na kuwawajibisha.
“Lakini pia wanafunzi wafidiwe fedha na muda
waliopoteza kwa wakati wote waliokuwa chuoni, kama hawatapewa haki zao, sisi
tutashirikiana na wadau wa elimu zikiwamo
asasi za utetezi wa kisheria
kutafuta haki mahakamani,” alisema Lusako.
Udom yazungumza
Ofisa uhusiano wa
Udom, Beatrice Baltazali alisema wanafunzi hao wote walifaulu vizuri wakiwa na
daraja la kwanza, pili na wachache daraja la tatu.
“Wanafunzi wote walikuwa na nafasi ya kwenda
kidato cha tano, lakini kwa kuwa waliahidiwa ajira, waliona wapitie huku kwa
kuwa watapata ajira ya moja kwa moja,” alisema.
Beatrice alisema walimu
wa Udom walikuwa wanalipwa fedha za ziada kuwafundisha wanafunzi wa programu
hiyo kwa kuwa walikuwa wanatumia muda mwingi zaidi ya kiwango walichokuwa
wamepangiwa.
“Kutokana na madai ya malipo hayo, mkaguzi wa
ndani aligundua kuna tatizo, ndiyo walimu nao wakaamua kugoma, wanafunzi wakawa
hawafundishwi Serikali ikaamua warudishwe nyumbani,” alisema Beatrice.
No comments:
Post a Comment