Wednesday, 22 June 2016

YANGA YAISHIKA PAZURI SIMBA SAKATA LA KESSY...HUENDA AKACHEZA DHIDI YA TP MAZEMBE


YANGA wamewaandikia barua Simba SC kuwajulisha kumsajili beki Hassan Ramadhan Kessy na kuuliza kama kuna pingamizi lolote kutoka kwao, na wakati huo huo nakala zimepelekwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).


Yanga ilishindwa kumtumia Kessy Jumapili katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika wakifungwa 1-0 na wenyeji MO Bejaia nchini Algeria, baada ya CAF kuomba barua ya kuruhusiwa kwake kuondoka klabu yake ya zamani, Simba SC, ambayo hawakuwa nayo. 
Hassan Kessy anaweza kuanza kuichezea Yanga SC wiki ijayo

Na mara baada ya mchezo huo, Yanga imewaandika barua mahasimu wao hao wa jadi, ikiwa imeambatanisha Mkataba wa Kessy na Simba ambao unaonyesha umemalizika Juni 15, mwaka huu na mchezaji huyo alikuwa sahihi kuingia Mkataba mpya na klabu nyingine.

Na Yanga imepanga iwapo hadi kufika Jumatano Simba haitakuwa na majibu yoyote ya barua hiyo – wataomba TFF iwasaidie kumuidhinisha beki huyo wa kulia kuanza kazi Jangwani, maana yake klabu yake ya zamani haitakuwa na pingamizi naye.

Na iwapo Simba SC watamuwekea pingamizi Kessy, watapaswa kuwa na hoja za pingamizi ambalo litasikilizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Richard Sinamtwa. 

Na kulingana na uzito wa suala hilo, inatarajiwa hadi kufika Ijumaa Kessy atakuwa amekwishapewa baraka za kuanza kuitumikia Yanga.

Wakati huo huo, winga wa kulia, Obrey Chirwa amefanikisha kupata vibali vyote vitakavyomruhusu kuanza kuichezea Yanga wiki ijayo katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Chirwa aliyesajiliwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe, aliondoka jana usiku Dar es Salaam kurejea Antalya, Uturuki ambako Yanga imeweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Jumatano dhidi ya TP Mazembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, klabu ya Mtibwa Sugar imetoa baraka zake kwa beki Andrew Vincent ‘Dante’ kuchezea Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika sawa na Coastal Union kwa Juma Mahadhi na Prisons kwa kipa Benno Kakolanya.

Wakati huo huo, kambi ya Yanga iliyopo mjini Antalya, Uturuki imekumbwa na mtikisiko kutokana na mabeki wote wa kushoto kupatwa na udhuru ambao unawaweka nje ya mchezo ujao dhidi ya Mazembe.

Oscar Joshua aliumia katika mchezo wa Jumapili na nafasi yake kuchukuliwa na Hajji Mwinyi kipindi cha kwanza, ambaye alikwenda kuonyeshwa kadi mbili za njano na kuwa nyekundu – maana yake hawezi kuhusishwa mchezo ujao na Mazembe.

Hadi jana Oscar alikuwa akiendelea na matibabu huku kukiwa hakuna dalili za kupona mapema na kuuwahi mchezo wa Jumatano. Na hao, Oscar na Mwinyi ndiyo mabeki pekee wa kushoto Yanga na hadi sasa haijafahamika kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm atafanya nini kuziba pengo hilo.


No comments:

Post a Comment