WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa
duniani ni kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa ni kubwa sana na linataka
juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo. (It’s a serious graft that needs
concerted efforts).
Ametoa kauli hiyo
mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Waziri wa Nchi wa Uingereza
anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Bibi Justine Greening walipokutana
kwenye mkutano huo uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.
Waziri Mkuu ambaye
alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, alimweleza
Bibi Greening kwamba viongozi wa Serikali wa awamu ya tano wameamua kwa dhati
kupambana na kila ovu linalotokana na janga la rushwa na pia wameamua kuwajibika
na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Sasa hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua
kufanya kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka utamaduni mpya
wa kupiga vita rushwa ili kuleta uwajibikaji na uwazi miongozi mwa watu wetu,” alisema.
Alipoulizwa ni kitu
kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa katika vita hii, Waziri Mkuu
alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo manne ambayo ni kuzuia rushwa isitolewe
ama kupokelewa (prevention), kampeni za kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya
sheria na kuwepo kwa utashi wa kisiasa.
“Serikali inachukua hatua za kiutawala na kisheria kama vile kuanzisha
mahakama maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai mwaka
huu,” alisema
Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Bibi
Greening alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano katika
kupambana na rushwa na kwamba ndiyo maana Tanzania ilipewa mwaliko maalum wa
kushiriki mkutano huo kwa vile baadhi ya mataifa yanaziona juhudi zinazofanywa
na Serikali.
Pia alitumia fursa
hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya awamu ya tano
imeionyesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza viwanda.
Pia alimhakikishia
Waziri Mkuu kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kwenye mpango wake
ilionao wa kupeleka umeme vijijini (Rural Electrification Programe).
“Tuko tayari kuwasiidia kutekeleza mpango huu kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema.
“Tuko tayari kuwasiidia kutekeleza mpango huu kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema.
Wakati huohuo, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya kimataifa, Bibi
Sarah Sewall ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya
rushwa na kusisitiza kwamba makampuni mengi ya Marekani yana nia ya kuja kuwekeza
Tanzania.
“Ninaamini uwekezahji huu utasaidia kuleta
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa watu wetu. Tunampongeza Rais Dk. Magufuli
kwa juhudi anazofanya na nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya
Tanzania na Marekani utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,”alisema.
Waziri Mkuu
alimshukuru Bibi Sewall na kumsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza wamarekani
wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi waje kuwekeza nchini katika
nyanja mbalimbali zikiwemo uanzishaji wa viwanda, uongezaji thamani kwenye
mazao yanayozalishwa nchini na kuhakiksha kuwa Watanzania wanajifunza
teknolojia mpya na za kisasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, MEI 14,
2016.
No comments:
Post a Comment