Wizara ya Nishati na
Madini imetengewa Sh trilioni 1.22 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 huku
fedha za miradi ya maendeleo zikiwa ni asilimia 94 ya fedha hizo.
Pia katika kuongeza
kiwango kikubwa cha uzalishaji wa nishati, kuongeza mchango wake katika Pato la
Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya Maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya
nishati.
Aidha, serikali
imeongeza bajeti ya maendeleo ya fedha za ndani kwa Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) kufikia Sh bilioni 534.4, huku wateja wa umeme wa REA na Tanesco
wakifikia 220,128. Mbali na hayo, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme
kimeongezeka kufikia asilimia 40.
Hayo yalisemwa bungeni
jana mjini Dodoma na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka
2016/17.
Profesa Muhongo
alisema bajeti ya wizara kwa mwaka 2016/17 ni Sh trilioni 1,22,583,517,000, na
kati ya fedha hizo, Sh 1,056,354,669,000 ni fedha za miradi ya maendeleo sawa
na asilimia 94.
“Kwa kuzingatia Ibara
ya 43(a) ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 inayoelekeza serikali kuongeza
kiwango kikubwa cha uzalishaji wa nishati ili kuongeza mchango wake kwenye Pato
la Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya Maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya
nishati,” alisema Profesa
Muhongo.
Alisema katika mwaka
wa fedha 2015/16, waliidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 642.12, na kati ya fedha
hizo, Sh bilioni 502.30 sawa na asilimia 78 ya bajeti yote zilikuwa ni bajeti
ya maendeleo.
“Hata hivyo, Bajeti hiyo iliongezeka kutoka
shilingi bilioni 642.12 hadi shilingi bilioni 762.12. lengo la ongezeko ni
kutekeleza miradi mikubwa ya kufua umeme ukiwemo Mradi wa Kinyerezi II – MW 240
ili kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini,” alisema Profesa Muhongo.
Megawati zaongezeka
Akizungumzia sekta
ndogo ya umeme, alisema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umeongezeka
kutoka megawati 1,226.24 Aprili, 2015 hadi kufikia megawati 1,461.69 Aprili, 2016
sawa na ongezeko la asilimia 19.
“Ongezeko hilo limechangiwa na mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia baada ya kukamilika kwa bomba la
kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam,” alisema.
Aidha, alisema mahitaji
ya juu ya umeme yameongezeka kutoka megawati 988.27 Desemba, 2015 hadi kufikia
megawati 1,026.02 Machi, 2016 sawa na ongezeko la asilimia nne.
Kuhusu upatikanaji wa
umeme nchini, alisema kiwango cha huduma ya upatikanaji wa umeme kimekuwa
kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Watanzania
waliofikiwa na huduma hiyo wameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi, 2015
hadi kufikia takribani asilimia 40 mwezi Aprili, 2016.
“Ongezeko hilo
limetokana na juhudi za serikali za kusambaza umeme nchini kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kuanzia Julai,
2015 hadi Aprili, 2016 idadi ya wateja waliounganishwa na umeme wa REA pamoja
na Tanesco ni 220,128 sawa na asilimia 88 ya lengo la kuunganisha wateja
250,000 ifikapo Juni mwaka huu.
Umeme bila MCC
“Katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme
vijijini, serikali imeongeza Bajeti ya Maendeleo ya fedha za ndani kwa REA
kutoka shilingi bilioni 357.12 kwa mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 534.4
kwa mwaka 2016/17. Tumeongeza asilimia 50 na hakuna fedha za MCC (Shirika la
Changamoto za Milenia) hapa,” alisema Muhongo.
"Ongezeko hilo ni kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020. Aidha, fedha za nje
zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo ni shilingi bilioni 53.21 sawa na asilimia
tisa na hivyo kufanya jumla ya bajeti yote ya REA kwa mwaka 2016/17 kuwa
shilingi bilioni 537.61.”
Mitambo
kuongezwa
Akizungumzia miradi ya
kuzalisha na kusafirisha umeme, alisema serikali itatekeleza miradi mingi
ambayo baadhi itakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Alisema katika juhudi
za kuongeza uzalishaji umeme, serikali imepanga kuongeza mitambo mingine ya
kuzalisha umeme ya Kinyerezi – I Extension wa megawati 185.
Alitaja mingine ni
Kinyerezi II megawati 240, huku akitaja miradi iliyo katika hatua za mwisho za
maandalizi ya miradi ambayo ni Kinyerezi III (megawati –MW 300), Rusumo Falls
MW 80), Malagarasi MW 45 na Kanoko MW 87.
Kuhusu miradi ya
usafirishaji umeme, alisema ujenzi wa mradi wa Iringa hadi Shinyanga wa
kilovolti 400 umefikia wastani wa asilimia 89, ambao gharama zake ni Sh bilioni
387.5 na utakamilika Septemba mwaka huu.
Alisema serikali
inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme zenye uwezo
mkubwa hususan kilovolti 400.
Miradi ambayo
utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2019/20 aliitaja kuwa ni
Singida – Arusha – Namanga kv 400, Bulyahulu – Geita kv 220, Geita – Nyakanazi
kv 220, North East Grid kv 400 na Somanga – Kinyerezi kv 400.
Aidha, alisema mradi
wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka
Somanga Fungu hadi Kinyerezi, Tanesco imeshakamilisha ulipaji wa fidia kwa
wananchi wanaopisha mradi huu.
“Hadi kufikia mwezi Aprili, 2016 shilingi
bilioni 26.06 tayari zimelipwa na Tanesco kwa watu 947 katika wilaya za Ilala
na Temeke,” alieleza.
Katika kuboresha miundombinu
ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, mwaka 2014 Tanesco ilianzisha
Kampuni Tanzu ya Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company Limited (TCPCO),
kwa ajili ya kujenga viwanda vya kutengeneza nguzo za zege nchini.
“Baada ya kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa
viwanda hivyo, TCPCO inatarajia kuanza uzalishaji wa nguzo za zege mwaka
2016/17,”alisema.
Kuhusu punguzo la
viwango vya bei za umeme, Profesa Muhongo aliliarifu Bunge kuhusu punguzo hilo
lililoanza Aprili mosi, mwaka huu.
Alisema serikali
imepunguza bei ya umeme kwa kati ya asilimia 1.5 na 2.4, na pia imeondoa tozo
ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na tozo ya huduma ya
mwezi ya Sh 5,520 kwa wateja wa umeme wa Daraja la TI na DI, ambao wengi wao ni
wa majumbani.
“Hatua hii itawasaidia
watumiaji wadogo wa umeme mijini na vijijini kumudu gharama hizo, hivyo
kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi,” alisema Profesa Muhongo aliyerejea katika
wizara hiyo baada ya kuwahi kuiongoza katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Kuhusu gesi asilia,
alisema kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia
Lindi hadi Dar es Salaam kumeongeza mchango wa uwezo wa mitambo ya kuzalisha
umeme kwa kutumia gesi asilia kufikia asilimia 49.
Aidha, alisema
uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia umewezesha gharama za uzalishaji
umeme nchini kupungua kutoka wastani wa Sh 262 hadi 229 kwa uniti moja ya
umeme.
Profesa Muhongo
alisema bomba hilo lenye urefu wa kilometa 542 ni pamoja na mitambo ya
kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Madimba (Mtwara) na Songo Songo (Lindi).
Mradi huo ulizinduliwa rasmi Oktoba, 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya
Kikwete.
Akizungumzia shughuli
za utafutaji gesi asilia, alisema Kampuni ya Dodsal imekamilisha tathmini ya
kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa katika kisima cha Mambakofi – I kwenye
Kitalu cha Ruvu Mkoa wa Pwani. Alisema tathmini hiyo inaonesha uwepo wa gesi
asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni (TFC) 2.17.
“Hivyo kufanya gesi asilia iliyogunduliwa nchini hadi Mei, 2016 kufikia
TCF 57.25 ikilinganishwa na TCF 55.08 zilizokuwepo mwezi Aprili, 2015. Kati ya
kiasi hicho, TCF 47.13 zipo kwenye kina kirefu baharini na TCF 10.12 zipo nchi
kavu,” alisema.
Akizungumzia
usambazaji wa gesi asilia jijini Dar es Salaam, alisema lengo la mradi huo ni
kujenga mtandao wa kusambaza gesi asilia kwa njia ya mabomba na iliyoshindiliwa
(CNG).
No comments:
Post a Comment